NEWS

25 Novemba 2019

Mgombea Ujumbe Serikali ya Mtaa Adaiwa Kuuawa


ALIYEKUWA mgombea wa Ujumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mnara wa Voda jijini Arusha, kwa tiketi ya Chadema, kabla chama hicho kujitoa, Sirili Homary amekutwa amefariki dunia nyumbani kwake eneo la Mnara wa Voda huku ikidaiwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni siku tatu zilizopita.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kifo hicho kina muda wa siku tatu tangu kimetokea.

Amesema mwili wa Marehemu Homary umekutwa ndani ya nyumba yake katika eneo la Mnara wa Voda, huku funguo ikiwa ndani na tayari akiwa amefariki Dunia.

“Bado tunachunguza na tutatoa taarifa kwa maana mtu amekutwa ndani na funguo ikiwa ndani inawezekana pia amejidhuru mwenyewe kutokana na labda msongo wa mawazo,” amesema Kamanda Shana.

Aidha, alisema wako wanasiasa wanaleta uchochezi juu la kifo hicho na ameahidi wakiendelea atawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

“Naomba watupe muda vyombo rasmi vya uchunguzi vifanye kazi yake, jambo kama hilo lina taratibu linapotokea tunachunguza kwa kuhusisha vyombo vinavyoaminiwa na Wananchi na tutatoa taarifa kupitia Vyombo vya Habari”amesema Shana.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema amesema jambo hilo ni la kikatili na la kuhuzunisha na kwamba amezungumza na Kamanda wa Polisi ambaye amemuambia watu kadhaa wanashikiliwa kuhojiwa juu ya mauwaji hayo.