NEWS

10 Novemba 2019

Rais wa Rwanda Paul Kagame Ajibu Tuhuma za Kuwapeleleza Wapinzani Wake ‘Natamani Kuwajua Adui zangu’ – Video


Raisi wa Rwanda Paul Kagame amejibu shutuma kuwa amekuwa akiwapeleleza wapinzani wake kupitia simu zao, amesema teknolojia inayohitajika kufanya hivyo ni ghali sana.



Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali siku ya Ijumaa, raisi Kagame amesema anatamani angekuwa na uwezo wa kununua teknolojia hiyo ”kujua zaidi” kuhusu adui zake.

Raia wa Rwanda anayeishi nchini Uingereza alisema kuwa anaamini kuwa alikuwa muathiriwa wa udukuzi uliofanyika kwa WhatsApp.

Faustine Rukundo alisema yeye na wafuasi wenzake wa chama cha Rwanda National Congress- kundi linaloipinga serikali ya Rwanda walikuwa wanalengwa kwa kutumia huduma za ujumbe.

Maabara ya Citizen, kundi la utafiti katika Chuo Kikuu cha Toronto, imethibitisha kuwa alikuwa anafuatiliwa.

WhatsApp imeishutumu Kampuni ya NSO Group kwa kuweka programu kwenye simu karibu 1,400 kwa nia ya kufanya upelelezi. Programu yake ya Pegasus inaweza kufanya kazi hiyo hata ikiwa mbali.

Idadi kubwa ya watu wanaofuatiliwa wanadaiwa kuwa raia wa Rwanda.

Kampuni ya NSO Group imekana madai dhidi yao, ikisema kuwa programu ya Pegasus imekuwa ikiuzwa kwa wateja waliohakikiwa na si wenye nia mbaya.

Mtandao wa WhatsAppWhatsApp ni moja ya mitandao mikubwa duniani inayotumia programu tumishi ya kutuma na kupokea ujumbe papo kwa kwa papo
Kilichotokea kwa Rukundo

Kwa miezi kadhaa Rukundo aliamini yeye na wenzake walikuwa kati ya watu karibu 1,400 waliokuwa wamelengwa na wadukuzi kupitia WhatsApp.

Lakini ilithibitishwa juma lililopita baada ya kupokea simu kutoka maabara ya Citizen mjini Toronto.

Kwa miezi sita, shirika lilikuwa likifanya kazi na Facebook kuchunguza udukuzi na kubaini walioathirika.

Watafiti wanasema ”Katika uchunguzi maabara ya Citizen imegundua visa 100 vya udhalilishaji vilivyowalenga watetezi wa haki za binaadamu na waandishi wa habari katika nchi karibu 20 dunani.

Bwana Rukundo aliyejipambanua kwenye ukurasa wake wa WhatsApp ni mkosoaji wa utawala wa Rwanda, sambamba na wengine wa kaliba yake walikuwa walengwa.

Mtandao wa udukuzi ulijengwa na kuuzwa na kampuni moja yenye makao makuu yake nchini Israel NSO na kuuza kwa serikali mbalimbali duniani.

LukundoFaustin Lukundo amedai kudukuliwa kupitia mtandao wa WhatsApp
Wadukuzi walitumia programu za kuwapeleleza waandishi wa habari, wanaharakati wa haki za binaadamu, lakini tukio hilo kwake liliifanya familia yake kuogopa mno.

”Kwakweli , hata kabla sijathibitiha hili, tulipigwa na butwaa na kuingiwa na hofu. Inaonyesha kuwa walikua wakiifuatilia simu yangu kwa karibu majuma mawili na waliweza kufikia kila kitu,” aliiambia BBC.

”Si tu shughuli zangu wakati huo lakini historia za mawasiliano yangu ya barua pepe na watu ninaowasiliana nao na kuzungumza nao.Kila kitu kilikua kinanaswa, Kompyuta, simu zetu, hakuna kilichokuwa salama.Hata tulipokua tukiongea, huenda walikua wanasikiliza pia.Bado ninahisi siko salama.”

Bwana Rukundo alitoroka Rwanda mwaka 2005 baada ya wakosoaji wa serikali kukamatwa na kutupwa gerezani. Alipambana ili mke wake aachiwe baada ya kutekwa na kushikiliwa kwa miezi miwili.

Facebook, mmiliki wa WhatsaApp, anajaribu kuishtaki kampuni ya NSO. NSO imekana shutuma dhidi yake. Programu hiyo ya simu inatumiwa na watu karibu bilioni 1.5 katika nchi 180.

VIDEO: