NEWS

23 Novemba 2019

Serikali Yasisitiza haiwezi kupanga bei elekezi ya mchele ama mahindi

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali haiwezi kupanga bei elekezi ya mchele ama mahindi hivyo amewataka wakulima kote nchini kupandisha bei ya mazao hayo kadri wawezavyo kulingana na mahitaji ya soko.

Akizungumza wakati alipotembelea kikundi cha wanawake wajasiriamali wauzaji wa mchele katika eneo la Vwawa Mkoani Songwe juzi tarehe 21 Novemba 2019 alisema kuwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya nafaka ambayo ni mahindi na mchele katika msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019 waendelee kunufaika na biashara ya mazao hayo kulingana na mahitaji ya soko.

Alisema kuwa wakati bei ya mazao hayo inaposhuka sokoni serikali haiingilii kupandisha bei ya mazao hayo na wananchi hufurahia kushuka kwa bei, hivyo basi wakati bei ikipanda pia wakulima wanatakiwa kuendelea kufurahia na kununua kwa wingi mazao hayo.

“Kuna watu wananipigia simu wakidai mishahara iongezwe kwa watumishi kwakuwa bei za mahindi na mchele zimepanda, na mimi nimekuwa nikiwajibu wakati bei ikipungua mbona hawajawahi kunipigia wakiniomba mishahara ipunguzwe” Alihoji Mhe Hasunga

Juzi Novemba 20, 2019 akizungumza na wananchi wa Gairo Mkoani Morogoro wakati akiwa safarini kuelekea Jijini Dodoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli aliwataka wakulima na wafanyabiashara kupandisha bei ya mahindi kutokana na hali ya soko huku akisisitiza kuwa serikali anayoiongoza haitopanga bei elekezi ya mahindi.

Alisema serikali anayoiongoza haiwezi kupanga bei elekezi ya mahindi kwani kufanya hivyo itakuwa imefilisika kiutawala, hivyo mahindi yatajiendesha kulingana na soko kwani huu ni mwaka wa wakulima hivyo wapandishe tu bei kadri wawezavyo kulingana na soko.

Mhe Rais alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa kwa mwananchi yeyote atakayeona mahindi yamekuwa ya bei ya juu aende akalime ya bei ya chini.

Aidha, Waziri wa Kilimo amesema kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kumkomboa mkulima ili kunufaika na jasho lake hivyo imnaendelea kuimarisha kitengo cha masoko ikiwa ni mkakati maalumu wa kuhakikisha kuwa wakulima wanajipatia kipato kizuri kwa kuwa na soko la uhakika la bidhaa za kilimo ndani na nje ya nchi.

MWISHO