NEWS

23 Novemba 2019

Tapeli akamatwa na kadi 23 za benki Akiwa Amezificha Sehemu za Siri

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM KUIMARISHA ULINZI KATIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limejipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani na utulivu.
 
Ndugu wana habari, tarehe 24/11/2019 ni siku ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji hivyo basi sisi kama Jeshi la Polisi tutaimarisha ulinzi maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam, katika vituo vya kupigia kura, ofisi zote za vyama vya siasa na ofisi zote za watendaji wa kata.
 
Aidha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi chochote cha watu watakao jaribu kuvuruga amani jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA WIZI WA FEDHA KWENYE MASHINE ZA KUTOLEA FEDHA (ATM) NA ATM KADI 23
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Bi Halima Juma (23)Mkazi wa Chalinze kwa tuhuma za wizi wa fedha kwenye mashine za kutolea fedha (ATM)
 
Mnamo tarehe 19/11/2019 katika benki ya CRDB tawi la Mbagala akiwa katika ATM hizo, aidha alimtilia mashaka binti huyo aliyekuwa kwenye chumba cha ATM ya benki hiyo akijifanya kuwasaidia wazee na wastaafu wasiojua kutumia ATM mashine vizuri, lakini lengo lake ni kuchukua namba za siri za wastaafu na wazee hao na kisha kuwabadilishia ATM kadi zao na baadaye kuwaibia fedha kwenye akaunti zao kwa kutumia kadi halisi za wahusika baada ya kuwabadilishia kadi na kuchukua namba za siri.
 
Mtuhumiwa huyo alikamatwa na askari wanaolinda Benki hiyo na alipopekuliwa alikutwa na ATM kadi 23 za watu mbalimbali za benki tofauti tofauti zikiwa katika pochi yake huku akiwa amezificha katika sehemu zake za siri ukeni.
 
Kadi hizo ni kama ifuatavyo;
1.CRDB kadi 07
2.NMB kadi 06
3.NBC kadi 02
4.AMANA kadi 02
5.POSTA BENKI kadi 02
6.ACB kadi 01
7.STANIBIC kadi 01
8.DTB kadi 01
9.EQUITY kadi 01
 
Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani hivi karibuni.

TAHADHARI YA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES SALAAM.​

Jeshi la Polisi kanda maalum Dar es salaam linapenda kutoa tahadhari kwa wakazi wa jiji la Dsm wote kuwa makini kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepukana na majanga yanayoweza kuepukika. 

Hivyo wananchi wote wanatakiwa kuwa makini na watoto wadogo wanaohitaji uangalizi wa karibu, pia kujiepusha kupita kwenye maji ya mito midogomidogo au madimbwi ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.
 
Aidha hadi sasa zimepokelewa taarifa za watu wawili kufariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

LAZARO .B. MAMBOSASA – SACP
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAM.