NEWS

9 Novemba 2019

Yanga Yaipiga Ndanda Bao 1-0

ILIWACHUKUA hadi dakika ya 73 mashabiki wa Yanga kusimama kwenye majukwaa yao na kushangilia kwa nguvu kubwa baada ya Patrick Sibomana kufunga bao la faulo nje ya 18. Yanga jana alikuwa mgeni wa Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

 

Ndanda ambayo ilipanda kucheza ligi kuu msimu wa 2014/15 imekuwa ikikaza kila inapokutana na Yanga pale Nangwanda na rekodi zinaonyesha zimekutana mara tano na Yanga imeshinda mara moja tu kama ilivyo kwa Ndanda huku zikitoka sare mara tatu.

Yanga, jana iliingia uwanjani ikiwa na benchi jipya la ufundi baada ya lile la awali lililokuwa likiongozwa na Mwinyi Zahera likitimuliwa. Waliokaa jana kwenye benchi ni Kaimu Kocha Mkuu, Boniface Mkwasa ambaye alikuwa na msaidizi wake, Said Maulid ‘SMG’.

 

Turejee uwanjani; Yanga ilianza mechi kwa presha kubwa huku ikipeleka mashambulizi mara nyingi kwenye lango la Ndanda lakini umakini wa mabeki wao waliituliza vyema safu ya ushambuliaji ya Yanga ilivyokuwa ikiongozwa na Sibomana na David Molinga.

 

Yanga ambayo kabla ya ushindi wa jana ilikuwa nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi saba ilizopata baada ya kucheza mechi nne ambapo kati ya hizo ilishinda mbili, sare moja na kichapo kimoja. Molinga na Sibomana ambao ndiyo mastaa wa Yanga, walionekana wakihangaika mbele ya lango la Ndanda na kupiga mashuti kadhaa ambayo mengine yalitoka na mengine kuokolewa.

 

Iliwachukua hadi dakika ya 73 Yanga kupata bao hilo kufuatia mpira wa faulo ambao ulipigwa kiufundi na Sibomana na kutinga nyavuni moja kwa moja huku ukimuacha kipa wa Ndanda Ally Mustapha ‘Barthez’ akiruka bila mafanikio. Faulo hiyo ilipatikana baada ya mchezaji wa Ndanda kuunawa mpira nje kidogo ya 18 ambapo awali alipiga Molinga lakini wachezaji wa Ndanda waliwahi kutokea na mwamuzi akaamuru irudiwe ndipo Sibomana akauingiza wavuni.

 

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa pia ulitawaliwa na rafu za hapa na pale kutokana na wachezaji kuonekana kukamiana, pia Issa Bigirimana wa Yanga alicheza kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa ligi kuu tangu ajiunge na kikosi hicho msimu huu na hakufanikiwa kugusa mpira. Kwa ushindi huo, Yanga inakwenda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo ikiwa na pointi 10.

 

METACHA AGEUKA KOCHA Kipa wa Yanga, Metacha Mnata, jana aligeuka kuwa kocha wa makipa ambapo alionekana akimnoa Farouk Shikalo. Yanga kwa sasa haina kocha wa makipa baada ya uongozi kuvunja benchi zima la ufundi na awali nafasi hiyo alikuwemo Peter Manyika.

 

Kikosi cha Yanga kilichoanza; Farouk Shikalo, Juma Abdul, Jafary Mohamed, Kelvin Yondani, Ally Mtoni, Papy Tshishimbi, Deus Kaseke, Mapinduzi Balama, David Molinga, Raphael Daud na Patrick Sibomana.

 

BABU SEYA AONGEZA MZUKA

Msanii wa Muziki wa Dansi, Babu Seya jana aliongeza mzuka kwa Yanga baada ya kuingia uwanjani na kuwahamasisha mashabiki wa Yanga kuishangilia timu hiyo na baada ya dakika chache tu Sibomana akafunga bao. Babu Seya alitinga uwanjani hapo akiwa na mwanaye Papii Kocha na msanii wa Bongo Fleva, Juma Nature.

STORI NA Sweetbert Lukonge

The post Yanga Yaipiga Ndanda Bao 1-0 appeared first on Global Publishers.