Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imemwekea vikwazo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Christian Makonda kwa madai ya kuhusika katika uvunjifu kamili wa haki za binadamu na tuhuma nyingine. Pia vikwazo hivyo amewekewa mke wake Makonda, Mary Felix Massenge.
Taarifa iliotolewa Ijumaa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeelezea tuhuma hizo ni uvunjaji wa haki za binadamu, ukandamizaji wa siasa za upinzani, ukandamizaji wa haki ya kujieleza na mikusanyiko, na kuwakandamiza watu ambao wanatengwa katika jamii.
Wizara ya Mambo ya Nje inasema ina taarifa zakuaminika kuwa Makonda alihusika katika uvunjaji wa amani katika nafasi yake kama mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.
Sheria ya Marekani inaagiza kuwa, katika hali ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ana habari za kuaminika kwamba maafisa wa nchi nyingine wamehusika na ufisadi mkubwa au ukiukaji wa haki za binadamu, watu hao na wana familia wa karibu hawataruhusiwa kuingia nchini Marekani.
Marekani inasema ina wasiwasi kwa kuendeleakukosekana uzingatiaji wa haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.
Hii ni pamoja na hatua ya serikali ya Tanzania inayochukua kukandamiza uhuru wa kujieleza, uhuru wa kujiunga na chama, uhuru wa mikutano ya Amani; kulengwa kwa watu wanaotengwa na vyama vya upinzani vya siasa, na hatarisho la maisha ya watu.