NEWS

2 Februari 2020

Watu 20 wapoteza maisha wakigombania 'mafuta ya upako' Kilimanjaro.. ....Jeshi La Polisi Lamtaha Mtume Boniface Mwamposa Ajisalimishe Haraka

Jeshi la Polisi limemtaka mtume Boniface Mwamposa kujisalimisha mwenyewe polisi kwa mahojiano kutokana na vifo vya watu 20 vilivyotokea mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro jana usiku Jumamosi Februari Mosi, 2020.

Watu hao walifariki usiku wakati waliposhiriki kongamano la kidini uwanja wa Majengo, wakigombea kukanyaga mafuta ya upako yaliyomwagwa milango ya kutokea uwanjani.

Wakati Jeshi hilo likimsaka kwa udi na uvumba kiongozi huyo wa kiroho, Jeshi hilo linawashikilia watu saba akiwamo mchungaji wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, Elia Mwambapa kwa mahojiano.

"Hatua tulizozichukua hadi sasa ni kuanza uchunguzi wa kujua ni nini hasa kilitokea na kupelekea vifo na majeruhi kwa hao waumini na tunawashikilia watu saba kwa mahojiano, Mchungaji Mwamposa tunamtafuta kwakuwa alitoweka mara baada ya hilo tukio kutokea" amesema Kamanda Hamduni.

Kwa mujibu wa Kamanda Hamduni jumla ya watu 20 walipoteza maisha siku ya jana ya Februari 1, 2020, katika viwanja vya Majengo Mjini Moshi, ambapo Watoto wa kike ni Wanne, Wanawake 15 na Mwanaume ni Mmoja, na majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Mawenzi.