NEWS

7 Septemba 2020

Mavunde: Waliopisha Ujenzi Uwanja Wa Ndege Wa Kimataifa Msalato, Ringroad Kuanza Kulipwa Fidia

Na Richard Mwaikenda, Dodoma
WANANCHI waliopisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato Dodoma, Barabara za Ringroad, wataanza kulipwa fidia hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde wakati wa uzinduzi wa kampeni kwenye viwanja vya Shule ya Chang'ombe, jijini Dodoma Septemba 5, mwaka huu.

Mpango huo ulipokelewa kwa nderemo na vigelegele na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo uliofurika umati mkubwa.

."Najua wananchi wengi mko hapa mnasubiri kwa muda mrefu kusikia kuhusu fidia ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato. Ndugu zangu tumekamilisha hatua zote za mwisho na uhakiki umekamilika, muda siyo mrefu tutaanza kulipa na wale watakaopisha Ringroad (Barabara za pete) nao watalipwa,"alisema Mavunde huku akishangiliwa kwa nguvu.

Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli, imetangaza kuanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kisasa eneo la Msalato Dodoma, utakaokuwa na uwezo wa kutua kwa mara moja ndege kubwa 17 aina ya Boing 787 Dreamliner na Airbus. Zimetengwa zaidi ya sh. Bil. 15 kulipa fidia kwa waliopisha ujenzi huo.

Mradi wa barabara za pete (Ring Roads) utahusisha ujenzi wa barabara ya mzunguko wa njia nne zenye urefu wa km 110.2 kwa kiwango cha lami kutoka Nala – Veyula – Ihumwa na Matumbulu. Shilingi bilioni 414 zitagharmia ujenzi wa barabara za pete (ring road) kwa kiwango cha lami na uboreshaji wa miundombinu katika Jiji hilo.

Mavunde aliwaomba wakazi wa jimbo hilo ifikapo Oktoba 28,2020, kumpigia kura ili akamilishe ujenzi wa visima vingi vya maji kwa lengo la kuwaondolea kero ya ukosefu wa maji.Wakati wa kipindi chake cha ubunge tayari keshajenga visima 11 kutoka mfuko wake binafsi.

Amesema endapo akichaguliwa yeye, Mgombea Urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli na madiwani 41 wa jimbo hilo, ameahidi kusambaza kompyuta katika shule zote za msingi na sekondari zilizomo jimboni humo.

Pia, Mavunde ameahidi kuandaa utaratibu wa kuwapatia mikopo wajasiriamali, wafanyabiashara ndogo ndogo, vijana, akina mama na walemavu.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mgombea Ubunge Jimbo la Kibakwe, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Steven Masele, wagombea ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile na Fatma Toufiq. Wote hao walipata wasaa wa kmnadi Mavunde, Dk. Magufuli na madiwani wa CCM.

Wengine waliohudhuria kampeni hizo ni; viongozi wa chama, waliogombea ubunge kwenye kura za maoni na kushindwa, wagombea udiwani Kata 41 zilizomo kwenye Jimbo hilo na wageni wengine waalikwa.