NEWS

1 Oktoba 2020

‘Tanzania Ni Nchi Kubwa, Inataka Kiongozi Mahiri’

“TANZANIA ni nchi kubwa inazidi kilometa za mraba 947,000. Ina makablia zaidi ya 120 na wakazi wake wanakaribia milioni 60. Inahitaji kiongozi mahiri na mwenye hofu ya Mungu.”

Hiyo ni kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa aliyoitoa jana (Jumatano, Septemba 30, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Ngara Mjini, kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya Posta, wilayani Ngara, mkoani Kagera.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Ngara, Bw. Ndayisaba George Ruhoro na mgombea udiwani wa CCM wa kata ya Ngara Mjini, Bw. Stanford Kennedy.

Akifafanua sifa za kiongozi anayetakiwa kuiongoza Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Tunataka tupate kiongozi mwenye hofu ya Mungu. Tanzania inahitaji kiongozi mahiri, mzalendo, mwadilifu na mwaminifu ambaye ni lazima tujiridhishe kuwa ataweza kuongoza nchi.”

“Nimeangalia katika wote wanaotaka kupewa Urais, hakuna kiongozi mwenye hizo sifa zaidi ya Dkt. John Pombe Magufuli. Tulimpa miaka mitano ya kuongoza nchi, amefanya mambo makubwa na nyote mmeona ama kusikia yaliyofanyika kupitia vyombo vya habari.”

Alisema Chama cha Mapinduzi ndicho chama pekee kinachoweza kuwatumikia Watanzania mpaka wale wanyonge, na akawaomba wakazi hao wawapigie kura wagombea wa CCM ili wawatumikie. “Dkt. Magufuli ni kiongozi ambaye anaweza kuiongoza nchi, ndiye kiongozi anaweza kuunda Serikali na kuisimamia ili iende ikawatumikie Watanzania mpaka wa chini kabisa kwa sababu ya uchapakazi wake. Ikifika tarehe 28 Oktoba, nendeni mkamchague kwa kura nyingi ili aendelee kuongoza,” alisisitiza.

Alisema Dkt. Magufuli ni kiongozi mwenye hofu ya Mungu aliyemtanguliza Mungu mbele katika kuleta mafanikio ya Taifa hili. “Kwa hiyo tunahitaji kiongozi mwenye hofu ya Mungu na ndiyo maana tulifanikiwa pia kupambana na vitu vingine vyote baada ya kumtanguliza Mungu. Kwani corona bado ipo?,” alihoji na kujibiwa hakuna.

“Hii ni kwa sababu ya kumuamini Mungu. Alitusihi Watanzania tufunge kwa siku tatu na tuombe kila mmoja kwa imani yake. Je hatujafanikiwa?” alihoji na kujibiwa tumefanikiwa.

Akielezea uboreshaji wa miundombinu ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema baada ya kukamilisha usanifu na upembuzi yakinifu, Ilani ya CCM ya 2020-2025 inatamka bayana kuwa barabara zinazounganisha wilaya hiyo na mji Bukoba kupitia Karagwe zitajengwa kwa kiwango cha lami.

“Barabara ya Lusahunga - Rusumo (km 92), Nyakanazi - Kobelo (km.60), Bugene -Kasulo (km.124) na Murugarama - Rulenge - Nyakahura (km 85) ziko kwenye mpango mahsusi ambao ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema.

Kuhusu maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa CCM itaendelea kuimarisha huduma za maji katika maeneo yote nchini lengo ni kuhakikisha kaulimbiu ya kumtua ndoo mama kichwani inatimia.

Mheshimiwa Majaliwa alisema katika wilaya ya Ngara, sh. bilioni 6.38 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya vijijini vikiwemo vijiji vya Makubu, Mbuba, Murugarama, Rwinyana, Kanazi na Kabelenzi, Murunyagira, Rusumo, Mshikamano, Kasharazi, Kasulo, Rwakaremela na Mugoma.

Alisema fedha hizo pia ziliwezesha ujenzi wa visima 23 kwa vijiji vya Kasulo, Kasharazi, Bukiriro, Rwakaremela, Nyakariba, Mwivuza, Mukubu, Kashinga, Kazingati, Bulengo, Chivu, Keza, Mbuma, Mukubu, Kashinga, Kigina, Nyamahwa, Nyamiyaga, Kanyinya, Murubanga, Kazingati, Nyarurama na Nyamahwa.

Alisema mradi uliosaidia wilaya ya Ngara kupata maji ni ujenzi wa miradi ya maji kutokana na fedha za mchango kwa jamii (CSR) kupitia mradi wa umeme wa Rusumo ambapo sh.  bilioni 11.5 zilitumika katika vijiji vya Kasulo, Rwakalemela, Mshikamano na Kasharazi.

(mwisho)