NEWS

23 Januari 2021

Corona yaua waziri wa tatu ndani ya wiki moja nchini Zimbabwe


Joel Matiza, Waziri wa Uchukuzi na Ustawi wa Miundombinu wa Zimbabwe ameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19, na hivyo kuwa waziri wa tatu kuaga dunia kwa maradhi hayo katika kipindi cha siku saba.

Waziri wa Habari wa Zimbabwe, Monica Mutsvangwa amethibitisha habari ya kuaga dunia Matiza akiwa na umri wa miaka 60. Amesema katika taarifa kuwa, "Covid-19 imeua waziri wetu mwingine, Mheshimiwa Joel Biggie Matiza, Waziri wa Uchukuzi na Ustawi wa Miundombinu."

Amesema mwanasiasa huyo alikuwa kada wa kutegemewa wa chama tawala na pia alikuwa mchapakazi ambaye alileta maendeleo makubwa katika sekta ya barabara nchini humo.

Matiza alifariki dunia jana Ijumaa, siku mbili baada ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo, Sibusiso Moyo kuaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19.

Januari 15, Ellen Gwaradzimbe, Waziri wa Masuala ya Mkoa wa Manicaland nchini Zimbabwe alifariki dunia kwa corona, miezi michache baada ya Perrance Shiri, aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Kilimo wa nchi hiyo kuaga dunia kwa maradhi hayo hayo ya kuambukiza.

Hadi sasa watu zaidi ya 30 523 wameripotiwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 nchini Zimbabwe tangu kesi ya kwanza ya ugonjwa huo iripotiwe nchini humo Machi mwaka jana, huku wengine 962 wakiaga dunia kwa ugonjwa huo.