Na. Saidina Msangi na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), amewaagiza wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuhakikisha Serikali inapata mafanikio makubwa Zaidi ya kukuza uchumi wan chi na kuboresha maisha ya wananchi.
Alitoa agizo hilo wakati akifungua Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Jijini Dodoma.
Alisema Watumishi wote wazembe, wavivu, wasio na nidhamu na wabadhirifu wa fedha za umma hawastahili kuwa katika Wizara hiyo na kumuagiza Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James asisite kutumia mamlaka aliyonayo kisheria kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wote wa aina hiyo.
“Nawasisitiza watumishi wote tufanye kazi kwa bidii, umakini na weledi ili kuharakisha maendeleo ya nchi kwani bado kuna kazi kubwa ya kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway- SGR), Umeme wa Maji – Julius Nyerere, pamoja na barabara za kuunganisha Tanzania na nchi jirani”, alisisitiza.
Aidha Waziri Mpango aliwaasa viongozi wa Wizara hiyo kujenga utaratibu wa kuwasikiliza watumishi wanaowaongoza ili kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko na manung’uniko ya wafanyakazi mahali pa kazi ili kuleta ufanisi.
“Uzoefu unaonyesha kuwa migogoro sehemu za kazi hujitokeza zaidi pale ambapo misingi ya ushirikishwaji, uwajibikaji na uwazi haifuatwi. Lazima tutambue na kukubali kuwa ufanisi sehemu za kazi hutegemea uhusiano uliopo baina ya viongozi na wafanyakazi,” alieleza Waziri Mpango.
Aliwasisitiza kuhakikisha masuala yote ya maendeleo ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na mahitaji ya mafunzo, upandishwaji vyeo, stahili zao pamoja na matatizo yao yanashughulikiwa kwa wakati ili kuleta ufanisi, tija na kudumisha nidhamu kazini na hivyo kuongeza ari ya wafanyakazi.
Kwa upande wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Waziri Mpango aliwaasa kutunza siri katika nafasi zao mbalimbali hasa kipindi hiki cha utandawazi na kuwa mtumishi yeyote atakayebainika kukiuka taratibu, miongozo na miiko ya kazi yake ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango atajutia ukaidi wake.
“Hatua ya kuendesha mikutano ya Baraza mahali pa kazi siyo tu kwamba ni utekelezaji wa sheria au kujipatia posho, bali ni fursa adhimu ya kuchochea mafanikio mahali pa kazi kwani Baraza la Wafanyakazi ni kiungo kati ya wafanyakazi na mwajiri,” alisisitiza Dkt. Mpango.
Waziri Mpango alieleza kuwa ni wajibu wa kila mjumbe kutekeleza majukumu yake katika Baraza hilo kwa ufanisi na nidhamu ya hali ya juu ili kufikia matarajio ya Wizara, Serikali na wananchi kwa ujumla na kusisitiza kila mjumbe awasilishe hoja za wafanyakazi wenzie na pia achangie mada zitakazowasilishwa ama kwa kuongea au kwa maandishi.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi alieleza kuwa vikao vya Bara za la Wafanyakazi vimekuwa na umuhimu mkubwa mahala pa kazi hivyo wizara inahakikisha vinafanyika mara mbili kwa mwaka.
“Miongoni mwa mafanikio ya Baraza la Wafanyakazi ni kuboreshwa huduma kwa watumishi, kuboreshwa kwa mazingira ya kufanya kazi ikiwemo kuwapatia watumishi vitendea kazi, kuelimishwa kwa wafanyakazi juu ya magonjwa sugu kama vile kisukari, homa ya ini na shinikizo la damu” alifafanua Bw. James.
Bw. James aliongeza kuwa Baraza la Wafanyakazi limekutana kwa lengo la uchaguzi wa viongozi baada ya waliokuwepo kumaliza muda wao na kuendesha mkutano wa kawaida utakaojadili utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita, kupokea na kujadili hoja za watumishi na mada mbalimbali kutoka ndani na nje ya wizara.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bi. Marry Maganga alimshuru Waziri wa Fedha na Mipango kwa kufungua Baraza hilo na kuahidi kuwa atasimamia utekelezaji wa maagizo yote aliyoyatoa ili kuhakikisha kazi zinafanywa kwa ufanisi na kufikia lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi.
Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi unafanyika katika kipindi ambacho Wizara ya Fedha na Mipango iko katika maandalizi Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambao ni wa mwisho katika utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2011/12 – 2025/26 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali.
Katika uchaguzi uliofanyika amechaguliwa Bw. Tumwesige Kazaura, kuwa Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Fedha na Mipango na Bi. Ellen Rwijage, kuwa msaidizi wake, ambao watadumu katika uongozi huo kwa kipindi cha miaka mitatu.