Mheshimiwa Sahle-Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Tanzania leo Jumatatu ya tarehe 25 Januari, 2021 kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Sahle-Work Zewde anatarajiwa kuwasili katika uwanja wa ndege wa Chato majira ya saa 4:00 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Baada ya mapokezi hayo ya Kitaifa, Mheshimiwa Zewde ataendelea na ratiba nyingine zitakazokuwa zimepangwa ikiwemo kufanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake.
Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili pamoja na kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa nchi zote mbili.
Profesa Palamagamba John Kabudi (Mb) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza na waandishi wa habari Chato, Mkoani Geita ameeleza kuwa, Tanzania na Ethiopia zimeendelea kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri wa muda mrefu. Uhusiano huo unatokana na msingi mzuri uliowekwa na Waasisi wa nchi hizi, Hayati Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Haile Sellasie wa Ethiopia ambao walishirikiana katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na uanzishwaji wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (Organization of African Unity -OAU) mwaka 1963.
Profesa Kabudi aliendelea kueleza kuwa Tanzania na Ethiopia zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kukuza lugha ya Kishwahili,uwekezaji, biashara, utalii, ulinzi na usalama, na usafiri wa anga.
"Mwaka 2017, nchi hizi zilisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) ya kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission of Cooperation-JPCC), Azimio la Pamoja la Mkakati wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia (Joint Declaration on Strategic Partnership between Tanzania and Ethiopia); na Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Utalii (Cooperation in Tourism) ambayo utekelezaji wake unaendelea vizuri". alieleza Profesa Kabudi.
Mashirikiano mengine baina ya Nchi hizi mbili ni pamoja na sekta ya Utalii,uchukuzi,ulinzi na Usalama, utamaduni pamoja na viwanda.
Takwimu za biashara kati ya Tanzania na Ethiopia zinaonesha ongezeko la kiwango cha biashara (Trade Volume) kati ya nchi hizi mbili. Mathalan kiwango cha biashara kiliongezeka kutoka Bilioni 1.5 mwaka 2012 hadi Bilioni 9.3 mwaka 2014 na kufikia Bilioni 13.5 mwaka 2019. Urari wa Biashara (Balance of Trade) uliongezeka kutoka Milioni 946.8 mwaka 2012 hadi Bilioni 12 mwaka 2019.
Aidha, taarifa ya Profesa Kabudi kwa waandishi wa habari imeeleza kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 13 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 14. 57 kutoka nchini Ethiopia katika kipindi cha kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 2020. Miradi hiyo imezalisha ajira 677 kwa Watanzania na ipo katika sekta za viwanda (manufacturing), ujenzi, uchukuzi na Utalii.
Tanzania ilifungua Ubalozi wake nchini Ethiopia tangu mwaka 1963, Ubalozi huo pia unaiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Afrika. Kwa kutambua umuhimu wa uhusiano wetu, Ethiopia nayo ilifungua Ubalozi wake hapa nchini mwezi Mei, 2018.