Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ina mpango wa kuongeza nguvu uzalishaji wa zao la alizeti kwa lengo la kuhakikisha kuwa kuna mafuta ya kutosha ya kula yanayozalishwa nchini na hivyo kupunguza utegemezi wa mafuta hayo kutoka nje.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo sasa uzalishaji wa ndani unakidhi asilimia 43. Aidha nchi inazalisha tani 270,000 za mafuta ya kula kila mwaka na huagiza nyingine tani 600,000 kufidia pengo lililopo ndani.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo leo mchana tarehe 22 Januari, 2021 wakati alipofanya ziara ya kukitembelea kiwanda cha kusindika mafuta ya kula ya alizeti; Kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania cha Jijini Dodoma.
Prof. Mkenda amesema kwamba pamoja na kuongeza nguvu kuhakikisha kwamba mafuta ya kula yanapatikana nchini kwa kiasi kinachotakiwa pia serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji na pia wakulima wadogo kuwa nafasi ya kusafirisha bidhaa zao nje.
Prof. Mkenda amesema kwamba anafahamu kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanasababishwa kukwama kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta nchini hivyo Serikali itapitia upya Sheria na kanuni ili kuondoa mkwamo na kuwezesha uzalishaji wa ndani kukua zaidi.
Waziri Mkenda alisisitiza kuwa hakuna mageuzi ya kiuchumi yanayoweza kutokea bila kuwa na mapinduzi kwenye kilimo.
"Tukiongeza tija kwenye kilimo, bei za bidhaa kama chakula itapungua, mageuzi kwenye kilimo yatasaidia sana kukuza viwanda hapa nchini.” Amesisitiza Prof. Mkenda.
Waziri wa Kilimo amesema suala la mbegu za alizeti ni changamoto lakini Serikaĺi itahakikisha mbegu za kutosha zinapatikana. Pia alitaka kuangaliwa kwa mfumo wa kilimo cha mkataba kwa kuboresha mfumo wake.
"Tabia ya Watu kuingia mkataba lakini wakati wa kuvuna wanampa mtu mwingine haipendezi, lazima Wakulima waheshimu mikataba.” Amekaririwa Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa ataitisha mkutano wa Wataalamu ili kuangalia upya sera na taratibu zinazotumika katika uzalishaji wa alizeti nchini.
Hata hivyo alikiri kwamba mahitaji ya mafuta ya kula nchini yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa corona ambao umesababisha mwenendo usiokuwa wa afya wa biashara ya kimataifa ikiwamo ya mafuta ya kula.
Waziri pia aliwaambia Wamiliki wa Kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania kwamba Serikali haijazuia upelekaji wa mafuta ya kula nje na kwamba kuchelewa kwa maofisa wa Serikali kutoa vibali kunaathiri Wakulima wadogo hapa nchini ambao wanategemea kiwanda kama hicho kupata soko la uhakika.
“Kiwanda hicho kimepata soko katika Jumuiya ya Ulaya ya kupeleka mafuta yaliyosafishwa mara mbili (Double Refined).”
“Tuna uwezo wa kuilisha nchi yetu na mafuta tunayozalisha wenyewe na kuuza mengine nje” alisema Profesa Mkenda na kuongeza kuwa kwa bahati mbaya Wakulima wadogo bado wanahangaika katika uzalishaji.
“Wataalam wanasema kama Wakulima wakibadilika na kufanya kilimo biashara chenye matumizi ya zana za kisasa na mbegu bora za kisasa wataweza kuzalisha tani 10 za alizeti kwa hekta.”
“Wakulima nchini wanazalisha chini ya tani moja kwa hekta.” Amekaririwa Waziri Mkenda.
Mkurugenzi Mtendaji kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania Bwana Malcolm McGrath alisema kiwanda chake kwa sasa kinazalisha tani elfu ishirini (20,000) kwa mwaka lakini kina uwezo wa kuzalisha mara sita zaidi ya hapo.
Mkurugenzi huyo amesema tayari wamekuwa na mawasiliano na Wakulima wadogo, wa kati na Wakubwa wa alizeti kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro, Manyara, Singida, Tabora na Kigoma lakini kuna changamoto kubwa ya ughali wa mali ghafi hivyo kufanya bidhaa yao kuwa ghali ukilinganisha na nchi nyingine zinazopeleka mafuta katika soko la Ulaya.
Bwana McGrath ameiomba Serikali kuwezesha kilimo cha mkataba ili wawe na uhakika wa mali ghafi na pia kusiwepo na uchelewefu wa usafirishaji wa bidhaa hiyo bandarini.
“Tunakabiliwa na changamoto za kuchelewa kwa makontena yetu bandarini. Pia bila sababu yoyote ile mamlaka za Manyara zimesitisha mpango wetu wa kufanyakazi na wakulima na hivyo hali hiyo itatuathiri kwa asilimia 25 ya malengo yetu,” alisema Mkurugenzi huyo.
Mwenyekiiti wa Shirikisho la Wachakataji Alizeti mkoa wa Dodoma Bwana Ringo Iringo amesema pia kuna changamoto katika masuala ya tozo mbalimbali na kodi ya ongezeko la thamani kwa teknolojia inayoingizwa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao; Wizara ya Kilimo Bwana Enorck Nyasebwa amesema timu ya Wataalamu itakutana kutafuta suluhisho la kuongeza uzalishaji nchini. Alisema kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya mafuta ya alizeti yanayozalishwa nchini katika soko la India na Afrika Kusini.
Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo la Taifa; Bwana Timoth Mmbaga amesema uhaba wa mafuta ya kula uwe ni onyo kwa nchi.
"Uhaba wa mafuta ya kula ni fursa pia ni onyo; Hivi Malaysia angekataa kutupa mafuta tungefanyaje? Ili ni onyo lazima tujitegemee na sasa tunajitosheleza kwa asilimia 43 tu. Jitihada zifanyike ili hii asilimia hiyo isirudi nyuma tena.” Amesisitiza Bwana Mbaga.