NEWS

9 Machi 2021

Mtendaji wa COSOTA Awashukia wanaoghushi hati za umiliki


Anitha Jonas – COSOTA, Dar es Salaam
Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Doreen Sinare atoa onyo kali kwa  Watayarishaji wa Filamu nchini wanaoghushi Hati ya Umiliki Halali wa Ubunifu  “Clearance Certificate”.

Mtendaji huyo ametoa onyo hilo leo Jijini Dar es Salaam katika mkutano  wa Multichoice Tanzania  uliolenga kutangaza fursa kwa Watayarishaji wa Filamu kuwasilisha andiko la  Uandaaji wa Filamu ambapo Multichoice watatoa ufadhili wa fedha katika kuandaa kazi hiyo.

Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo Bibi. Doreen alisisitiza kuwa hivi sasa ofisi yake tayari imeanza kutumia Kanuni ya Ufifilishaji, hivyo kwa wale watu wote watakao kamatwa wakifanya uharamia wa kazi za Sanaa wataadhibiwa kwa kanuni hii ambapo  watahitajika kulipa faini isiyopungua milioni ishirini.

“Kumekuwa na baadhi ya watoa huduma za “Cable” kuwa na tabia ya chukua chaneli/vipindi zikiwemo filamu na tamthilia kutoka visimbuzi vingine au kutumia njia nyingine kurusha cable zao bila idhini ya wamiliki ya wamiliki wa maudhui hayo hili ni kosa sababu ni wizi na ukiukwaji  wa Hakimiliki,”Bibi.Doreen.

Kwa upande wa Meneja Masoko na  Mahusiano Multichoice Tanzania Bw.Ronald Shelukindo alisema utaratibu wa kupokea Maandiko ya Filamu utanza  kuanzia tarehe Machi 08 hadi 14, 2021 na maombi hayo yatawasilishwa kwa njia ya tovuti, lengo la kuwasilisha kazi hizi kwa njia ya mtandao ni kuepuka malalamiko kuhusu watu wa kati au  dhana ya Multichoice hutoa nafasi kwa kujuana.

“Uongozi wa Multichoice Tanzania unapenda kutoa pongezi kwa serikali kwa namna unavyotoa ushirikiano na kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya kushirikiana.”alisema Shelukindo.

Akiendelea kuzungumza Bw.Shelukindo alisisitiza kuwa moja ya vitu vitakavyozingatiwa  wakati wa uchambuzi maandiko hayo ni kuwepo kwa cheti cha umiliki wa ubunifu wa kazi hiyo kutoka COSOTA.

Pamoja na hayo nae Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dkt.Kiagho Kilonzo aliwasihi wadau wa tasnia ya filamu nchini kuacha malumbano, badala yake  wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.

Vilevile Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Filamu Bw.Denis Sweya aliomba uongozi wa Multichoice kubadili lugha ya mikataba yao na kuwa kwa lugha ya Kiswahili ili wadau waweze kusaini wanachokielewa.

Katika kuhakikisha suala la tafsiri kwa lugha ya Kiswahili katika mikataba ya Multichoice linafanikiwa na kufanyiwa kazi kwa haraka COSOTA ilitoa ushirikiano kwa kuwasiliana na Baraza la Kiswahili Tanzania  BAKITA, ambapo Multichoice waliridhia kuwasilisha nakala ya mkataba huo Machi 09, 2021 kwa ajili ya kuweza kutafsiriwa .

Halikadhalika Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Taifa Bw.Salum Mchoma alitoa ombi kwa uongozi wa Multichoice kutoa mafunzo kwa waigizaji ili waweze kufanya vyema katika kazi zao sababu wao ni watu wa mwisho katika mchakato wa uandaaji wa filamu ila ni watu muhimu  katika kukamilisha kazi hiyo na kuonesha ubora wa kazi hiyo.