NEWS

12 Machi 2021

Thailand yasitisha matumizi ya Chanjo ya Corona- 'AstraZeneca' kupisha tathmini zaidi


Thailand leo imejiunga na mataifa kadhaa ya Ulaya kusitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca kutokana na wasiwasi kuwa inasababisha kuganda kwa damu, licha ya baadhi ya mamlaka za afya duniani kusisitiza kwamba chanjo hiyo ni salama. 

Mshauri wa Kamati ya Taifa ya Kusamimia Chanjo ya Virusi vya Corona nchini Thailand amesema wanalenga kujiridhisha kuhusu usalama wa chanjo hiyo kabla ya kuitoa kwa umma na kwamba taifa hilo halina sababu ya kuwa na haraka. 

Kufuatia uamuzi huo, Thailand pia imesitisha mpango wa kumpatia chanjo ya AstraZeneca Waziri Mkuu Prayut Chan-O-Cha katika tukio ambalo lingerushwa moja kwa moja na televisheni nchini humo. 

Mataifa kadhaa ya Ulaya ikiwemo Denmark, Norway, Iceland, Italia na Romania yalitangaza jana kusitisha kwa muda au kupunguza usambazaji wa chanjo ya AstraZeneca baada ya kuwepo ripoti ya kuganda kwa damu kwa baadhi ya watu waliopatiwa chanjo hiyo.