NEWS

10 Machi 2021

Watendaji waagizwa kuwashughulikia watakaosababisha Moto kichaa


Na Amiri Kilagalila,Njombe
Watendaji wa kata za halmashauri ya mji wa Njombe wameagizwa  kusimamia sheria na kumshughulikia mtu yeyote atakayesababisha moto kichaa wakati wa maandalizi ya mashamba kwa ajili ya kilimo au katika shughuli yoyote kutokana na hasara kubwa ambazo hutokea mara baada kutokea kwa moto katika maeneo yao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizobainishwa na baadhi ya watendaji wa kata tano za tarafa ya Igominyi katika mdahalo wa wakulima ulioandaliwa na shirika la mwamvuli wa matumaini (Highland hope Umblella HHU) mjini Njombe ni kwamba zipo sababu za uchomaji moto hovyo ikiwemo uchomaji wa mkaa pamoja  wafanyakazi wanaopewa majukumu ya usimamizi wa uendelezaji wa mashamba ya  kilimo cha miti na parachichi kushindwa kulipwa posho zao na wawekezaji.

Aidha wamesema Kata tatu za Ihanga,Yakobi na Kifanya tarafa ya Igominyi ni miongoni mwa kata zinazoongoza katika usababishaji wa moto kichaa ukilinganisha na kata zingine 13 za halamshauri ya mji wa Njombe

“Kwenye kata yangu moto huwa unatoroka kila mwaka kipindi cha kiangazi kwa hiyo tumeendelea kuweka mpango mkakati kwa ajili ya kufuatilia wote wanaochoma moto bila kibali”Devother Poul Mtendaji wa Yakobi

Mtendaji wa kata ya kifanya amesema “Kata ya kifanya ni miongoni wa kata zinazochoma moto na kuahribu uchumi wa wananchi wetu hii changamoto imeleyta shida sana,kikubwa nilichojifunza hapa ni hawa wenzetu wanaosimamia mashamba ya miti wakati mwingine inafika wakati hawajalipwa posho zao mpaka wanachukua maamuzi magumu”

Kwa upande wake Bethseba Liduke mkurugenzi wa shirika Mwamvuli wa matumaini,kupitia mdahalo huo ametoa rai kwa wakulima kubadirika na kuacha mfumo wa kuchoma moto ili kuandaa mashamba kwa kuwa zipo njia mbali mbali za maandalizi ya shamba.

“Wakulima tunahitaji kubadirika,mfumo wa kuchoma moto kabla ya kulima umepitwa na wakati,majani tunayochoma ni mbole inayohitajika katika shamba ni wajibu wetu wakulima kuachana na hii habari kwasababu ni uvivu wa kufukia nyasi kwa faida ya udongo”Beth Liduke Mkurugenzi wa shirika la mwamvuli wa matumaini (HHU)

Afisa wa mifugo na uvuvi Ndug,Thadei Luoga kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya mji,amewataka watendaji wa kata kuzingatia na kusimamia sheria kama zinavyoelekeza ili kudhibiti changamoto ya moto kabla na baada ya kuanza kilimo.

“Sheria iko wazi ukikutwa na tukio la moto faini yake ni laki tatu (300,000/= T’sh) unaweza ukatozwa faini peke yake au faini pamoja na kifungo cha zaidi ya miezi sita.Sasa bahati mbaya viongozi wengi huko kwenye kata hatusimamii sheria”alisema Thadei Luoga

Luoga amepongeza kata ya Liwengi pamoja na kata nyingine za halmashauri hiyo kwa kufanikiwa kupunguza changamoto za uchomaji moto ukilinganisha na baadhi ya kata huku wakiendelea kukua katika sekta ya kilimo.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji Njombe, Stanley Mayemba amepongeza hatua ya shirika la HHU kubaini changamoto zinazowakabili wakulima na kuwahakikisha kuwapa ushirikiano zaidi ili mkulima aweze kunufaika na kilimo chake.