NEWS

17 Juni 2021

Rais Samia Ashuhudia Utiaji Saini Mikataba Mitano Ya Ujenzi Na Ukarabati Wa Meli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akiwa jijini Mwanza ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitano kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya nne pamoja na ukarabati wa meli moja ya abiria uliofanywa na Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na wakandarasi wa meli hizo.

Akizungumza baada ya zoezi la utiaji saini wa mikataba hiyo mitano, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia MSCL kwa kazi nzuri ya ukarabati mkubwa wa meli mbili za New MV Butiama na New MV Victoria, pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo ambayo tayari imeanza kutumika kujengea meli mpya ya MV. Mwanza ‘Hapa Kazi Tu.”

“Tumeshuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ya ujenzi wa meli, hii ni kazi nzuri ya kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye ndie muanzilishi wa kazi hizi, ametuacha akiwa amezianza nasi tunaziendeleza, napenda niwahakikishie kwamba Serikali itahakikisha miradi mitano iliyotiwa saini leo na yenyewe itamalizika kama ilivyo kusudiwa”, amesisitiza Rais Samia

Ameongeza kuwa Serikali inadhamira ya kuufanya mkoa wa Mwanza kuwa kitovu kikubwa cha biashara kati ya nchi za maziwa makuu na ndio maana Serikali inajitahidi kujenga miundombinu bora ya bandari, reli na barabara zinazo unganisha Mwanza na mikoa mingine pamoja na kujenga kiwanja cha ndege na kununua ndege mpya.

Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amemshukuru Rais Samia kwa kufungua miradi mikubwa ya ujenzi wa Reli ya Kisasa pamoja utiaji saini wa mikataba mitano ya ujenzi wa meli itakayokuza uchumi wa mkoa wa Mwanza na kuufanya kuwa  kitovu cha biashara ya usafirishaji wa mizigo kutoka Tanzania kwenda nchi jirani kwa kupitia njia ya maji na barabara.

“Mheshimiwa Rais, baada ya wewe kuufungua Mkoa wa Mwanza kiuchumi vilevile umefungua shughuli za kiuchumi katika mkoa wa Kigoma, meli mbili kati ya tano ambazo mikataba ya ujenzi wake imesainiwa ni kwa ajili ya Ziwa Tanganyika, hivyo kwa mara ya kwanza Kigoma itaona meli mpya na hiyo ni faraja kubwa kwa wakazi wa mkoa huo pamoja na mkoa jirani wa Katavi”, amesema Dkt. Chamuriho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu,  Mheshimiwa Selemani Kakoso, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri za ujenzi wa Taifa zinazoendelea kufanyika, ameongeza kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Bajeti ya shilingi Bilioni 135 kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya malipo ya awali ya miradi mipya ya ujenzi na ukarabati wa meli kwenye Ziwa Victoria, Tanganyika pamoja na Bahari ya Hindi.

“Mheshimiwa Rais hiki kinachofanyika leo ni historia kubwa ndani ya Serikali ni imani yangu kuwa watanzania sasa wanaona kwa vitendo ahadi yako ya mwendelezo wa kazi zilizotanguliwa na mtangulizi wako Hayati Dkt. John Pombe Magufuli”, Mheshimiwa Kakoso.

Mikataba hiyo mitano iliyosainiwa inathamani ya shilingi Bilioni 438.8, ambayo ni mkataba wa ujenzi meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 2800 itakayotoa huduma katika Bahari ya Hindi, meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 3000 itakayotoa huduma Ziwa Victoria, meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 2800 itakayotoa huduma Ziwa Tanganyika, meli mpya itakayobeba abiria 600 na mizigo tani 400 itakayotoa huduma Ziwa Tanganyika pamoja na mkataba wa ukarabati wa Meli ya MV. Umoja inayotoa huduma katika Ziwa Victoria.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi