NEWS

19 Mei 2022

Benki ya Dunia yatenga dola bilioni 30 kukabili mgogoro wa chakula uliosababishwa na vita vya Ukraine


Benki ya Dunia imetangaza kuwa, imetenga dola bilioni 30 za misaada kwa ajili ya kudhibiti mgogoro wa chakula duniani uliosababishwa na vita vya Ukraine.

Shirika la habari la IRNA limeripoti hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, Benki ya Dunia imetangaza kwamba misaada hiyo itajumuisha dola bilioni 12 za kuendesha miradi mipya na zaidi ya dola bilioni 18 za kuendeleza na kukamilisha miradi iliyopo ya kudhamini chakula.

Benki hiyo ya dunia aidha imesema, miradi mipya itaekezwa kwenye kilimo, kukabiliana na athari za kuongezeka bei za vyakula kwa watu maskini na miradi ya maji na kilimo cha umwagiliaji.

Misaada hiyo mingi itatolewa kwa nchi za Afrika, nchi za Asia Magharibi, Ulaya Mashariki, Asia ya Kati na Asia Kusini, maeneo ambayo ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na vita vya Ukraine.