Waziri wa Madini Dotto Biteko ameiagiza Ofisi ya Madini Mkoani Kigoma kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza kuona uwezekano wa kuanzisha soko la madini ya chumvi Wilayani humo ili kutoa nafasi kwa wakazi hususani wa kipato cha chini kunufaika na rasilimali hiyo inayopatikana kwenye maeneo yao.
Maelekezo hayo yametolewa kufuatia maombi ya wananchi wa halmashauri hiyo kulalamikia ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa hiyo na kuiomba Serikali kufanya utaratibu wa kulifungua kuwawezesha kufanya biashara yao mahali salama.
Biteko alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na uongozi wa Kiwanda cha Chumvi Uvinza alipokitembelea baada ya kufanya mazungumzo na wananchi ambao pamoja na mambo mengine, walilalamikia malipo duni kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kujadili na kufikia uamuzi wa kuongeza ujira kwa wafanyakazi hao hadi kufikia Agosti mosi.
Wananchi pia walilalamikia uongozi wa kiwanda hicho kuuza chumvi inayozalishwa hapo kwa bei kubwa inayowafanya wafanyabiashara kupata faida kidogo.
Biteko aliutaka uongozi wa kiwanda hicho na wachimbaji wengine wa chumvi wilayani humo, kupunguza bei ya bidhaa hiyo ili kuiwezesha jamii inayowazunguka kunufaika na uwepo wa chumvi katika mji wao.
Alisema mtu mwenye kurekebisha bei ya chumvi kwa manufaa ya wafanyabiashara wadogo ni mwekezaji mkubwa.
“ifanye jamii hii iugue siku ukiwa haupo, ifanye jamii ikukumbuke kwa mema yako,” alisema Biteko.
Pia aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Uvinza, Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Kigoma pamoja na uongozi wa kiwanda kukutana kujadili mahali patakapofaa kuanzisha soko la madini ili kuwaondolea adha ya soko la chumvi wananchi wa Uvinza.
Kufuatia malalamiko ya wananchi wa Uvinza ya kutozwa Sh 500 ya ushuru kwa kila kilo 25 za chumvi, Biteko aliiagiza halmashauri hiyo kufuta tozo hiyo na kueleza kuwa haipo chini ya mamlaka yake na hivyo haitambui.
Katibu wa Wachimbaji Wadogo wa Wilaya ya Uvinza, Hamisa Kambi, alisema moja ya changamoto yao ni maeneo yao kuvamiwa, ukosefu wa vitendea kazi, halmashauri kutowapa kipaumbele wamiliki wa leseni kwenye tenda za Serikali na kuomba kurahisishwa kwa utolewaji vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi.