Rais Hollande
Trierweiler, ambaye ni First Lady asiyetambulika kisheria, amealikwa kumsindikiza Hollande kwenye ziara hiyo ambapo watafikia ikulu ya White House.
Mwanamke huyo amelazwa tangu Ijumaa kutokana na kuwa na msongo wa mawazo uliotokana na kusambaa kwa habari kuwa rais Hollande, 59, ana uhusiano wa siri na Julie Gayet, 41.
Alipoulizwa kama Trierweiler bado ni First Lady wa Ufaransa, Hollande alisisitiza kuhusu haki yao ya maisha binafsi. “Nalielewa swali lako na nina uhakika utaelewa jibu langu,” alisema. “Kila mmoja katika maisha yake binafsi hupitia vipindi vigumu. Hicho ndicho kilichopo kwangu. Huu ni wasaa mgumu. Lakini nina kanuni moja: Masuala haya binafsi hushughulikiwa faragha. Huu si muda ama mahali pa kufanya hivyo hivyo sitajibu swali lolote kuhusu maisha yangu binafsi.”
Akijibu swali la hali ya Trierweiler, Hollande alisema: “Anapumzika na sina mengi ya kusema.”
Marafiki na viongozi wengine wamemtaka Hollande kuweka wazi haraka kama bado ana uhusiano na Trierweiler. Hata hivyo amekataa kutangaza hadharani uamuzi waliochukua wapenzi hao kuhusu mustakabali wao. Nao marafiki wa Trierweiler wamenukuliwa na vyombo vya habari vya Ufaransa kuwa yupo tayari kumsamehe Hollande kama akimpiga chini Gayet.