Hii ni kwa wale walio ndani ya ndoa na wale wanaotarajia kuingia kwenye ndoa. Ukiona ndoa imedumu kwa miaka mingu siyo bure na ndiyo maana leo nimeona niwaletee mbinu 3 madhubuti ambazo zinaweza kuifanya ndoa yako idumu milele.
Muamini, akuamini!
Uaminifu ni kitu cha msingi sana kwa wanandoa, unaposhidwa kumuamini mwenza wako mara nyingi sana utakuwa ukidhan anakusaliti kwa kuwa na mtu mwingine hata kama unavyodhani vinaweza vikakosa ukweli ndani yake.
Hali hiyo inaweza kukufanya ukakosa raha kila mwenza wako anapokuwa mbali na wewe. Si kukosa raha tu anapotoka ama anapokuwa mbali na upeo wa macho yako bali pia anaporudi unaweza kushindwa kuonesha upendo wako kwake na kuweza kujenga chuki dhidi yake.
Amini kwamba mwenza wako ni mwaminifu kwako na jijengee mazingira ambayo na yeye ataamini kwamba wewe ni mwaminifu kwake. Muamini ili naye akuamini. Epuka sana kufanya mambo ambayo yanaweza kumsababishia mwenza wako akadhani una uhusiano wa kimpenzi na mtu mwingine nje ya ndoa.
Waweza kufanya hivyo kwa kuwa makini na maneno yako pamoja na matendo yako ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kudhihirisha kwamba siyo mwaminifu katika ndoa.
Kitendo cha kuchelewa kurudi kazini kila siku bila kuwa na sababu za msingi, kulala nje, kuwa na uhusiano wa karibu na watu jinsia tofauti bila kuwepo na sababu za msingi, kupunguza mapenzi, kutokuwa na heshima ni baadhi ya matendo ambao yanaweza kuonesha kwamba siyo mwaminifu hivyo ni vyema ukaepukana navyo.
Usiwe mbishi
Watu wana tabia tofauti. Kuna wengine wana tabia ya ubishi hata kama jambo linalozungumziwa halistahili ubishi. Kama utakuwa na tabia hiyo basi ni vyema ikaishia nje ukiwa unabishana na wenzako kwa kufurahisha genge.
Tambua kwamba mabishano hayana nafasi katika ndoa.
Unapokuwa na tabia ya kubishana na mpenzi wako hata katika kile ambacho hakistahili kubisha, fahamu unakaribisha mazingira ya kuwepo kwa ugomvi.
Kama kweli unataka kuona ndoa yenu inakwenda vizuri jifunze ukweli kwamba siyo kila wakati unaweza kuwa sahihi, kuna wakati utakuwa hauko sahihi na inapotokea hivyo basi kubaliana na hali halisi kisha omba msamaha.
Wazazi wetu wamekuwa mara nyingi wakitufundisha kwamba kumbishia mtu aliyekuzidi umri ni dalili za kutokuwa na heshima.Hivyo hivyo kwa wanandoa, unapombishia mwenza wako inaonesha kwamba haumheshimu tabia ambayo inaweza kusababisha nyufa katika ndoa yenu.
Maneno ya watu ni sumu
Hivi unajua kwamba kuna baadhi ya watu hawapendi kuwaona wenzao wakiwa katika ndoa yenye furaha na amani?Watu hawa ndiyo wanaosababisha kuvunjika kwa ndoa nyingi. Maneno ya watu ndiyo yamekuwa yakijenga ama yakibomoa ndoa nyingi hivyo basi sikushauri usiyasikilize kabisa, japo yapo yenye maana.
Anapokuja mtu na kukuambia amemuona mume wako ama mke wako na mtu mwingine, kwanza jiulize mtu huyu ana lengo gani? Hivi lengo lake siyo kukutaka umuache kweli, endelea kujiuliza kwamba ndoa yenu ikivunjika ama ikiwa katika machafuko yeye aliyekuletea taarifa hizo atafaidika na nini? Kwa kifupi hakuna.
Ndiyo maana nasema, unayoambiwa na watu yachuje kwanza kabla ya kuyafanyia kazi sio kila unaloambiwa unakimbilia kuchukua uamuzi. Maneno ya watu mara nyingi yanasababisha kuvunja ndoa za wengi kama siyo kusasabisha machafuko katika ndoa hivyo ni vyema ukaepukana nayo.
Kabla ya kumalizia mada hii niseme kwamba kumekuweo na malalamiko ya mara kwa kwa wanandoa ambao wote wanafanya kazi juu ya uaminifu.Tunafahamu kwamba ikitokea bahati mkaoana wote mnafanya kazi uvumilivu wa hali ya juu unahitajika bila uvumilivu ndoa itavunjika mara moja.
Ndiyo maana tumekuwa tukishuhudia ndoa za watu matajiri zikiwa katika matatizo makubwa.