HII ni aibu ya baba mchungaji! Mchungaji wa Kanisa la Elgibbon Ministry lililopo Songwe mkoani Mbeya, Imani Kalinga amejikuta akipata aibu ya aina yake baada ya kufumwa laivu na mkewe akifunga ndoa na mwanamke mwingine mrembo (kifaa) aliyefahamika kwa jina la Bupe Kajigili.
NI JUMAMOSI ILIYOPITA
Tukio hilo lililozua taharuki kwa waumini waliokuwa wakifuatilia ibada hiyo ya ndoa, lilitokea Jumamosi iliyopita ambapo mchungaji huyo alimuacha mkewe Mbeya na kuja jijini Dar kufunga ndoa na mwanamke huyo katika kanisa moja lililopo Kibamba Kibwegele.
TAARIFA ZA AWALI
Awali, ilidaiwa kuwa mchungaji Imani alikuwa na mgogoro wa ndoa na mkewe Elizabeth Jeremiah ambapo kesi yao ilitakiwa kutolewa uamuzi na Mahakama ya Mwanzo ya Mbalizi, Machi 5 mwaka huu ambapo kabla ya tarehe hiyo, mchungaji huyo akaamua kutaka kuoa bila kumtaarifu mkewe.
MKE ATONYWA
Wakati mchungaji huyo akiwa kwenye mipango yake ya siri, wapambe walimtonya mkewe kuwa mumewe alikuwa Dar kwa ajili ya kufunga ndoa na mwanamke mwingine.
Taarifa hizo zilimshtua mwanamke huyo ambaye alifunga safari toka Songwe mpaka Dar akiwa ‘jeshi’ lake na kufanikiwa kumkuta mumewe akiwa madhabahuni na Bupe huku vigelegele na wimbo wa ‘wanameremeta’ ukiwa umetawala kanisani hapo.
MKE AVAMIA
Baada ya kushuhudia hayo, Elizabeth alivamia madhabahuni na karatasi za mahakamani na vielelezo lukuki kuhusu ndoa yao ambapo alimuonesha Mchungaji Steven Jungwa aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo.
Mchungaji Jungwa ambaye anadaiwa kumfahamu vizuri mchungaji mwenzake Imani na mkewe Elizabeth, alianza kurushiwa lawama na mwanamke huyo aliyekuwa akimtuhumu kumjua kwa muda mrefu kama ndiye mke halali wa mchungaji Imani na hata nyumbani kwao ameshawahi kuishi nao lakini alikubali kumfungisha Imani ndoa na mwanamke mwingine.
MCHUNGAJI JUNGWA KIMYA
Mchungaji Jungwa hakuwa na la kuzungumza zaidi ya kumung’unya maneno na kisha kusema alikuwa hawafungishi ndoa isipokuwa alikuwa akiwabariki.
MAJIBU YAZIDI KUTIBUA
Majibu ya Mchungaji Jungwa yalimfanya mwanamke huyo azidi kuwa mbogo na kuwaanzishia kasheshe hapohapo madhabahuni.
AHAMIA KWA MAMA MKWE
Elizabeth baada ya kuwavaa maharusi hao, aliangalia mabenchi ya mbele na kumuona mama mdogo wa bwana harusi aitwaye Anna Yona ambapo naye alimvaa na kumshutumu kuwa mama mkwe mnafiki anayejua kuwa mwanaye ana mke, watoto na wajukuu naye lakini amekubali kutoroka kutoka Mbeya kuja Dar kuhudhuria ndoa hiyo.
Katika varangati hilo, mama mkwe huyo aliyekaa na dada wa bwana harusi waliishia kushika tama wakati wakisemwa na mkwe wao Elizabeth.
MCHUNGAJI KIONGOZI AINGILIA
Katika kunusuru machafuko, mchungaji kiongozi wa kanisa hilo aliingilia kati sakata hilo kwa kuwaomba watu watulie ili barua hiyo ya mahakama isomwe vizuri kanisani hapo.
Kijana mmoja aliisoma barua hiyo iliyoonesha walikuwa na mgogoro wa ndoa na kwamba walitakiwa kufika mahakamani Machi 5, mwaka huu kujadili ndoa hiyo.
Alipofika kwenye kipengele hicho, waumini wote walisikika wakimlaumu bwana harusi huyo kufunga ndoa hiyo kabla ya tarehe ya shauri hilo.
NDOA YAKWAMA
Baada ya hapo mchungaji kiongozi aliamrisha ndoa hiyo ivunjwe na maharusi hao watarajiwa na watu wengine wote watawanyike.
Akizungumza na wanahabari wetu, Elizabeth alisema kinachomuuma ni kwamba wametoka mbali sana na mumewe huyo ambapo wamebahatika kupata watoto wanne na wajukuu wawili.
“Mbaya zaidi mume amechukua ng’ombe wangu nasikia ndiyo amekwenda kumlipia mahari hiyo mwanamke. Yaani inaniuma sana,” alisema mwanamke huyo.
Gazeti lilizungumza na mchungaji aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo ambapo alisema yeye alikuwa hawafungishi ndoa isipokuwa alikuwa akiwabariki kwakuwa walishaanza kuishi.
Wanahabari wetu walipokuwa wakitaka kuwahoji maharusi, mpambe wa bibi harusi aliwavamia na kuwanyang’anya kamera kitendo kilichozua purukushani nyingine kanisani hapo huku msimamizi wa bwana harusi naye akichimba mkwara.
Hata hivyo, hawakufanikiwa kuwapora kamera waandishi na pia waandishi wetu hawakufanikiwa kuhojiana na bwana harusi huyo.
Imeandikwa na Richard Bukos na Issa Mnally.
Stori: WAANDISHI WETU
The post AIBU YA BABA MCHUNGAJI AMTOROKA MKEWE, AENDA KUOA ‘KIFAA’ appeared first on Global Publishers.