NEWS

20 Februari 2018

BAADA YA KUJIFUNGUA, MKE WA AZORY: NISAIDIENI NATESEKA!

Mke wa Azory.

 

WAKATI leo ni siku ya 92 tangu kupotea kwa mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda, mke wa mwandishi huyo, Anna Pinoni (36), hali yake sio mzuri baada ya kujifungua kwa operesheni katika Kituo cha Afya, Kibiti mkoani Pwani wiki iliyopita na ameomba asaidiwe.

 

Gazeti hili lilifika Kibiti, Ijumaa iliyopita mchana lakini halikufanikiwa kukutana na mama huyo baada ya kuelezwa kuwa hataweza kuongea na mwandishi wetu kutokana na hali yake kutokuwa mzuri.

 

Hata hivyo, Jumamosi iliyopita lilifanikiwa kuzungumza na Anna kwa taabu hospitalini hapo ambapo alisema kuwa kikubwa zaidi anachokiomba ni msaada kutoka kwa Watanzania wenye upendo ili aweze kuishi na mwanawe huyo mchanga na mwingine mdogo.

 

“Naomba nisaidiwe sina kazi, sina mume wa kuweza kusaidiana kutunza hawa watoto, kwa sasa maisha yangu yanahitaji kusaidiwa ili niweze kuyamudu na hawa watoto, namshukuru Mungu huyu mtoto mchaga hana matatizo, ni mimi tu hali yangu bado mbaya, mwili umevimba, naomba nisaidiwe,” alisema mama huyo kwa uchungu.

 

 

Akiwa na kichanga chake.

 

Naye dada wa Anna, Paskazia Pinoni (pichani) alimwambia mwandishi wetu kuwa baada ya kujifungua kwa operesheni mdogo wake ghafla usiku hali yake ilibadilika na mwili ulimvimba, hali iliyowatia wasiwasi.

 

“Kwa kweli hali yake siyo mzuri, bado amelazwa baada ya kujifungua kwa operesheni lakini ghafla usiku hali yake ilibadilika kuwa mbaya kwani mwili ulimvimba sana, tunawashukuru sana madaktari kwa jinsi wanavyomshughurikia mgonjwa wetu,” alisema dada yake huyo.

 

Aliongeza kuwa waliambiwa na madaktari kuwa hali hiyo ilitokana na msongo wa mawazo aliokuwanao Anna kwa kumuwazia mume wake Azory kila akifikiria kwani kwa sasa hana kazi na mumewe amechukuliwa na watu wasiojulikana katika mazingira ya kutatanisha na ana mtoto mchanga na mwingine mdogo, haelewi ataishinao vipi.

 

Kipindi Azory amepotea kwa utatanishi mkewe huyo alikuwa na ujauzito wa miezi sita huku akifanya shughuli zake za ushonaji hapo hapo Kibiti lakini kwa sasa ofisi hiyo ya ushonaji ameifunga na hana tena sehemu ambayo inamsaidia kupata kipato.

 

 

Azory.

 

TUJIKUMBUSHE

Kwa mujibu wa mkewe Anna, Novemba 21 mwaka jana asubuhi, watu wasiojulikana wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walifika katikati ya mji wa Kibiti sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara na kumchukua.

 

Baada ya kumchukua Azory, gari hilo lilielekea shambani kwake saa nne asubuhi na kumkuta mkewe huyo akiwa huko.

Imeelezwa kuwa Azory aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma alimuita mkewe kutokea upande huo wa gari na kumuuliza alikokuwa ameuweka ufunguo wa nyumba yao.

 

Taarifa ilisema mkewe alilisogelea gari na kuzungumza naye kutokea dirishani na kumwelekeza alipoficha ufunguo, huku Azory akimwambia amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo Novemba 21, basi angerudi siku inayofuata Novemba 22 (mwaka jana.)

 

Gari hilo liliondoka kwa kurudi kinyumenyume hadi njia panda na kuelekea nyumbani kwa mwandishi huyo. Mkewe aliporudi nyumbani aligundua kuna upekuzi ulifanyika kwa sababu alikuta vitu viko shaghalabaghala.

 

Tangu siku hiyo, imeelezwa Azory hajaonekana na namba zake tatu za simu za mkononi hazipatikani. Novemba 23, mkewe Anna alitoa taarifa Kituo cha Polisi Kibiti na jalada lake kupewa RB namba; Kibiti/RB/1496/2017.

 

Imeelezwa polisi waliahidi kufanya uchunguzi, lakini mpaka sasa hakuna taarifa zilizotolewa.

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii na angependa kumsaidia mke wa Azary anaweza kuwasiliana naye kwa simu namba 0713 939 597 au 0754 389 600.

STORI: ISSA MNALLY, PWANI

The post BAADA YA KUJIFUNGUA, MKE WA AZORY: NISAIDIENI NATESEKA! appeared first on Global Publishers.