NEWS

19 Februari 2018

Baba wa Akwilina atamani kukutana na Polisi Aliyempiga Risasi Mwanaye ili Amng'ate hata Meno Tu

Akwilini Shirima ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyepigwa risasi na polisi Februari 16, 2018 amesema siku akikutana na askari aliyemuua mwanaye atapambana naye hadi kifo.

Akizungumza leo Februari 19, 2018 nyumbani kwake Kijiji cha Olele, Shirima alisema endapo muuaji atakuwa ni kijana mwenye nguvu kumzidi, atapambana naye hata kwa kumuuma kwa meno.

"Najua ni ngumu kukutana na aliyempiga mwanangu risasi, lakini laiti ningekutana naye kama ni kijana mwenye nguvu kunizidi nitapambana naye hata kumuuma kwa meno,” amesema.

“Kama ni mzee mwenzangu nitapambana naye hadi kifo ila kwa bahati mbaya siwezi kumpata, hivyo sina namna. Kwa kweli hiki kifo kimezima ndoto ya familia ya kuondokana na umasikini.”

Shirima ameiomba Serikali kuliangalia suala hilo kwa kina na kuona namna ya kumsaidia kwa kuwa tegemeo lake limeondoka na wao kwa sasa hawana msaada wowote na wanachosubiri ni kifo.

"Jamani hii ni taa yangu imezimika na kuniacha gizani kwani toka nimepata taarifa za kifo chake sijaweza kula chochote. Nimekuwa kama nguruwe aliyetelekezwa porini bila msaada," amesema.

"Nilipopata taarifa za kifo cha mwanangu nilishtuka sana na kuhoji ni mwizi au nini kimetokea, lakini baadaye nikaambiwa ni Serikali imefanya mambo hayo. Imenitia uchungu sana na siwezi hata kula"

Shirima amesema ni afadhali mwanaye angeugua akamuuguza kuliko kifo cha ghafla alichokipata ambacho kimewaacha kwenye hali ambayo haitafutika mioyoni mwao katika maisha yao yote.

Mama wa marehemu, Costanzia Akwilini amesema mauaji ya mwanaye ni ya kinyama na bora angekuwa mbuzi angekula nyama kujifariji kuliko kwa mwanaye ambaye hakuna anayeweza kumfuta machozi.

"Mwanangu hakuwa mwanasiasa ameuawa akiwa kwenye gari akielekea kwenye shughuli zake, familia tulijinyima tukajichanga kwa kushirikiana na majirani ili asome aje atukomboe,” amesema.

“Leo nasubiria niletewe maiti kwenye jeneza. Kwa kweli imeniuma sana na kunikatisha tamaa. Naomba Serikali itende haki katika tukio hili," amesema mama wa marehemu katika mahojiano hayo.

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.

Credit: Mwananch