KIKOSI cha Yanga, kimeondoka jana asubuhi kwenda Shelisheli kwa ajili ya mechi yake ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St Louis.
Hata hivyo, Yanga imeondoka nchini bila kuwa na mshambuliaji wake wa kutumainiwa, Mzambia, Obrey Chirwa, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni majeruhi. Inadaiwa ana maumivu ya misuli.
Hata hivyo, Kocha Msaidizi wa Yanga,
Shadrack Nsajigwa, amewatoa hofu wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuwa, watashinda mechi hiyo hata bila ya kuwa na Chirwa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Nsajigwa alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi hiyo kwa hiyo anaamini kwa wachezaji walioondoka nao, wataiongoza timu hiyo kupata ushindi.
“Watu wengi walishitushwa na taarifa za Chirwa kutokuwepo katika mechi yetu ya marudiano na St Louis, lakini wanapaswa kujua kuwa mchezaji huyo siyo pekee ambaye hucheza uwanjani.
“Kwa hiyo, kuna mchezaji ambaye tumemwandaa ili kuziba nafasi hiyo na tunaamini atafanya vizuri, niwaombe tu wapenzi na mashabiki wetu kutokuwa na hofu na hilo, tutafanya vizuri,” alisema Nsajigwa.
Katika msafara wake huo, Yanga pia imewaacha Amissi Tambwe, Yohana Nkomola, Donald Ngoma, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Thabani Kamusoko ambao ni majeruhi.
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam.
The post KOCHA YANGA: TUTASHINDA BILA CHIRWA appeared first on Global Publishers.