NEWS

21 Februari 2018

MWENYEKITI, MWANASHERIA MISUNGWI WAKAMATWA

Mwenyekiti  wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Anthony Bahebe, akiwa chini ya ulinzi baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) jijini Mwanza leo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu  wa fedha za umma.

 

JESHI la Polisi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) imemkamata Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Anthony Bahebe.

 

Pia Mwanasheria wa Halmashauri hiyo,  Alphonce Sebukoto,  naye amekamatwa. Viongozi wote hao wanakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha za umma.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema kukamatwa kwa viongozi hao kunatokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.

 

Aliongeza kwamba  Bahebe amekamatwa leo na wote wanaendelea kuhojiwa na Polisi kwa kushirikiana na TAKUKURU.

 

Naye Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Makale alisema Sebukoto aliidhinisha malipo ya sh.milioni 278 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye ni Bahebe.

 

Alisema Sebukoto aliidhinisha malipo hayo kwa  Bahebe Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi ambapo jumla sh. milioni 138 ziliingizwa katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti huyo. Alisema kiasi kingine cha fedha kinachunguzwa kubaini kilipo.

 

Februari 19, 2018 akiwa katika ziara yake wilayani Misungwi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alimsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi,  Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.

 

Alichukua hatua hiyo baada mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vyema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 278.

 

Amesema mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh.milioni 278 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Anthony Bahebe.

 

Waziri Mkuu alisema Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji wa Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim.

 

Alisema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.

 

Alisema Mwanasheria alimlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri,  jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

 

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

 

 

 

 

The post MWENYEKITI, MWANASHERIA MISUNGWI WAKAMATWA appeared first on Global Publishers.