BAADA ya juzi Jumamosi Simba kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere, amefunguka kuwa, ni mwanzo mzuri kwao na wanaona wana kila sababu ya kubeba mataji mengine yaliyopo mbele yao.
Kauli hiyo ya Kagere ni kama kuitisha Yanga ambayo hivi sasa inajipanga kuhakikisha inarudisha makali yake na kubeba ubingwa wa ligi kuu au Kombe la FA ili mwakani ishiriki michuano ya kimataifa.
Katika mchezo huo wa juzi uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagere alifunga bao la kwanza kwa Simba huku Hassan Dilunga akifunga la ushindi. Lile la Mtibwa lilifungwa na Kelvin Sabato.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kagere alisema ubingwa wao huo ni kama deni ambalo wanapaswa kulilipa kwa mashabiki katika kuchukua mataji mengine zaidi.
“Tunashukuru Mungu kwa kuanza msimu vizuri, huu ni mwanzo mzuri kwetu na inatufanya
tuongeze juhudi kabisa kuhakikisha tunatwaa mataji mengine yote yaliyopo mbele yetu,” alisema Kagere na kuongeza:
“Kwa takriban mechi mbili sikufunga, lakini leo (juzi) nimefanikiwa kufunga, ni jambo zuri na mara nyingi huwa siingii uwanjani kuangalia nitafunga mabao mangapi, bali naangalia nitaisaidia vipi kwanza timu, ndiyo maana kuna baadhi ya mechi sikufunga lakini hatukupoteza.”
Said Ally, Dar es Salaam
The post Kagere Aitisha Yanga SC appeared first on Global Publishers.