NEWS

17 Agosti 2018

Risasi Zarindima Mahakamani na Kumjeruhi Mmoja

Risasi zimerindima katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, wakati askari magereza mmoja akijaribu kumzuia mtuhumiwa ambaye alikuwa ameachiwa huru.

Moja ya rasasi hizo ilimpata Gabriel Msuya (19), mkazi wa wa Mabibo Jeshini, ambaye alikuwa amefika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake.

Tukio hilo lililotokea jana saa tano asubuhi, lilizua taharuki na watu kutawanyika kwenye eneo.

Baada ya kupigwa risasi, Msuya alikaa takribani dakika 15 akiwa amelala chini huku akiwa amezungukwa na askari.

Msuya alisikika akilalamika kuwa na maumivu, huku akiwaomba askari hao kumpeleka hospitali.

Baadaye alipandishwa katika gari la polisi na kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala ambako alikaa kwa muda kabla kuhamishiwa Hospitali ya Mloganzila iliyopo Kibamba wilayani Ubungo.

Kabla ya kuchukuliwa na kupelekwa hospitali, mmoja wa askari hao alisikika akisema; “unaona sasa, haya ndiyo madhara, watu mnaachiwa mnakimbia ovyo.”

Baadaye askari aliyerusha risasi hizo, aliondolewa eneo hilo na polisi.

Kabla ya kuondoka, walifika askari kanzu ambao walitaka kumchukua, lakini walizuiwa na askari magereza wengine.

Mtuhumiwa aliyekuwa ameachiwa huru na mahakama, risasi zilivyopigwa alilala chini na baada ya hali kutulia walimkamata.

Hata hivyo, askari hao hawakutaka kutaja jina la mtuhumiwa huyo wala sababu za kutaka kumkamata tena baada ya kuwa ameachiwa huru.

Credit: Mtanzania