HOFU imetanda baada ya beki wa kulia wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Shomari Kapombe kuumia katika mazoezi yaliyofanyika juzi jioni wakati akijiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika mwakani nchini Cameroon.
Taifa Stars kesho Jumapili inatarajiwa kupambana na Lesotho, kwenye Uwanja wa Setsoto uliopo Maseru, Lesotho kuanzia Saa 11:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki ukiwa ni mchezo wa Kundi L.
Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Kapombe aliumia juzi Alhamisi katika mazoezi ya jioni kwenye kambi ya timu hiyo iliyokuwa Bloemfontein, Afrika Kusini.
Alisema, sababu kubwa ya kuumia kwa Kapombe ilitokana na kuukanyaga mpira vibaya jambo ambalo lilimsababishia maumivu makali ya kifundo cha mguu.
“Baada ya kutokea kwa tukio hilo madaktari wa timu wakiongozwa na Richard Yomba wamejitahidi kumtibu, lakini hajapata nafuu na kuna uwezekano mkubwa wa kutocheza mechi hiyo,” alisema Msangi.
Kutokana na hali hiyo, beki wa kulia wa timu ya Nkana FC ya Zambia, Hassan Kessy ndiye anayetarajiwa kuchukua nafasi hiyo ya Kapombe.
Said Ally, Lesotho
The post Kapombe apatwa na balaa Sauzi appeared first on Global Publishers.