NEWS

31 Desemba 2018

WAZIRI MKUU AZINDUA TAWI LA BENKI YA CRDB RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Tawi la Benki ya CRDB la Ruangwa. Kushoto ni mkewe Mary, wapili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Ally Hussein Laay na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Tawi la Benki ya CRDB la  Ruangwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Tawi la Benki ya CRDB la  Ruangwa.

Jengo la Benki ya CRDB tawi la Ruangwa ambalo lilozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi kompyuta mpakato Kiongozi wa Chama cha Msingi cha Umoja 2017, Omari Hassani Magoma  baada ya kuzindua tawi la Benki hiyo la Ruangwa.

Kiongozi wa Chama cha Msingi cha Umoja  2017 wilayani Ruangwa, Omari Hassan Magoma akionyesha Kompyuta Mpakato aliyokabidhiwa. 

Baadhi ya waalikwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Majaliwa wakati alipozindua Tawi la Benki ya CRDB la Ruangwa.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua tawi la benki ya CRDB wilayani Ruangwa na kuushukuru uongozi wa benki hiyo kwa kuwa tawi hilo litahamasisha ukuaji wa uchumi pamoja na kuwawezesha wananchi kujua umuhimu wa kuhifadhi fedha zao benki.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema ni vema kwa benki ya CRDB ikasogeza huduma hususan kwa wananchi waishio katika miji mikubwa iliyo mbali na makao makuu ya wilaya kwa kufungua ofisi za uwakala na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Desemba 31, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuzindua tawi la benki ya CRDB, ambapo ametumia fursa hiyo kuwahamisha wananchi kutumia benki kwa kuhifadhi fedha zao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kwa sasa benki hiyo inatakiwa itoe mikopo midogo, ya kati na mikubwa  kulingana na uhitaji wa wajasiriamali ndani ya wilaya hiyo kwa sababu mikopo itawawezesha wananchi waweze kukuza mitaji na kujikwamua kiuchumi.

Pia Waziri Mkuu ameipongeza benki ya CRDB kwa kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli katika kuboresha maendeleo ya sekta mbalimbali zikiwemo za afya pamoja na elimu kupitia misaada mbalimbali inayotolewa na benki hiyo nchini.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki ya CRDB imekua na kupanua wigo wake wa kufikisha huduma kwa wateja na kuunga mkono sera ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za fedha.

Alisema tawi hilo ni la sita katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania, kwani tayari wanamatawi mengine manne ambayo ni Lindi mjini, Mtwara, Masasi, Tandahimba na tawi  linayotembea katika Wilaya ya Newala. Pia wapo katika hatua za mwisho za ujenzi wa tawi Nachingwea.

“Wilaya hii ya Ruangwa ni kiungo muhimu sana katika uchumi wa mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla, hivyo uwepo wa mfumo rasmi wa kibenki,  kupitia  tawi hili la Benki ya CRDB, utasaidia sana kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kufungua fursa mpya.”

Mkurugenzi huyo alisema CRDB wanajivunia utendaji mzuri wa tawi hilo, kwani katika kipindicha mwaka mmoja toka limeanza kazi, limeweza kupata matokeo makubwa ya kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa amana ambazo zimefikia kiasi cha shilingi bilioni 1.5.

 

Pia jumla ya AMCOS 12 wanachama 4,600 zimejiunga na kufungua akaunti zao hivyo kuongeza usalama wa fedha zao. Pia  jumla ya mikopo ya shilingi bilioni 1.2 imeshatolewa kwa wateja wa wilaya hiyo, ambapo shilingi milioni 409 zilitolewa katika kilimo cha korosho na ufuta, wakati shilingi milioni 790 zilitolewa kama mikopo kwa wafanyakazi na wafanyabiashara.

Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

The post WAZIRI MKUU AZINDUA TAWI LA BENKI YA CRDB RUANGWA appeared first on Global Publishers.