NEWS

1 Januari 2019

Rais Magufuli awatakia heri ya mwaka mpya 2019 Watanzania wote

Rais Magufuli awatakia heri ya mwaka mpya 2019 Watanzania wote
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewatakia heri ya Mwaka Mpya wa 2019 Watanzania wote na kuwaomba wadumishe umoja, amani na upendo waliouonesha katika mwaka 2018.

Akizungumza kutoka nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amesema mwaka 2018 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Watanzania na anatarajia kuwa mwaka 2019 utakuwa wa mafanikio zaidi kulingana na mipango ambayo nchi imejipangia kuitekeleza.

Mhe. Rais Magufuli amewataka watumishi wa umma, viongozi, wakulima, wafanyabiashara, wavuvi na wafugaji kuongeza juhudi za uzalishaji mali katika mwaka 2019 huku wakipiga vita rushwa, wizi, ufisadi, ubadhilifu na kwamba anaamini kuwa uchumi wa Tanzania utazidi kupanda katika mwaka 2019.

“Ujumbe wangu kwa watumishi wa umma, ni kama nilivyotoa ujumbe kwa Watanzania wengine, wachape kazi, wajiamini, waachane na utamaduni wa kila kitu wanachokifanya kudai ni maagizo kutoka juu, huo ni ugonjwa ambao umeanza kuwapata watumishi wa umma ambapo kila wanalolifanya hata kama ni kwa mujibu wa sheria hawataki kujiamini, na wanasema hili ni maagizo kutoka juu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Amemalizia kwa kusema; “Ninaanza kuiona Tanzania mpya inakuja, tusiiachie Tanzania mpya, tuifike, tuikae na tuiishi kwa sababu huu ndio wakati wa kuijenga Tanzania mpya, nina imani kubwa sana Mungu wetu atatusaidia, mwaka 2019 mengi mazuri yatafanyika, kikubwa ni mshikamano wetu sote Watanzania, niwaombe Watanzania wote wa rika zote, wa dini zote, wa makabila yote, mshikamano waliouonesha kwa mwaka 2018 katika Serikali, wauoneshe tena mwaka 2019, na ikiwezekana wauoneshe zaidi na zaidi kwa kutanguliza zaidi uzalendo na Utanzania wetu, tutafanikiwa, Mungu ni mwema, Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki Watanzania wote na Mungu ubariki mwaka 2019.