NEWS

2 Januari 2019

Simba, Yanga Kutua Zanzibar Kibabe Leo

TIMU za Simba na Yanga zinatarajia kuelekea visiwani Zanzibar leo kwa ajili ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyoanza kutimua vumbi Januari Mosi.

 

Yanga ambayo ipo Kundi B, inatarajia kushuka dimbani Januari 3 dhidi ya KVZ huku timu nyingine zilizo kundi moja ni pamoja na Azam, Malindi na Jamhuri ya Pemba na kwa upande wa Simba inayotarajia kushuka dimbani, Januari 4 dhidi ya Chipukizi, ipo Kundi A ikiwa pamoja na timu nyingine za KMKM na Mlandege.

 

Michuano ya Kombe la Mapinduzi imeanza kutimua vumbi jana Januari Mosi kwa timu kadhaa kushuka dimbani ambapo inatarajiwa kufikia tamati Januari 13, huku zawadi za washindi zikiongezwa kutoka milioni 10 hadi milioni 15 pamoja na medali za dhahabu.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa timu hizo, walieleza kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya vyema katika michuano hiyo huku kwa upande wa Simba wakieleza kuwa inashusha kikosi kamili kwa ajili ya kujiandaa na mechi za Caf.

Msemaji wa Simba Haji Manara alisema: “Tunatarajia kuondoka Dar kesho (leo) kuelekea Zanzibar na tutashusha kikosi chote kwa kuwa tunatumia nafasi hii kwa ajili ya kujiandaa na mechi za makundi Caf, hivyo ni nafasi nzuri kwetu kujiandaa,” alimaliza.

 

Aidha, kwa upande wa Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema: “Sina kikosi kamili, Makambo (Heritier) amekwenda Congo, wengine 10 wana matatizo mbalimbali, wachezaji waliobakia ni 20 hivyo hatutapeleka kikosi cha kwanza.”

 

Aidha, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh ameeleza kuwa kikosi kinaondoka leo saa nane mchana na wachezaji 11 akiwemo mlinda mlango mpya, Hamidu Abdulrahman, Deus Kaseke, Haji Mwinyi, Said Juma ‘Makapu’, Anthony Mateo, Mustapha Simon, Maka Edward, Thaban Kamusoko, Juma Mahadhi, Pius Buswita, Jaffary Mohamed, Juma Abdul, Cleofas Sospeter pamoja na kipa wa U-20 Ibrahim Abrahaman.

 

The post Simba, Yanga Kutua Zanzibar Kibabe Leo appeared first on Global Publishers.