NEWS

2 Aprili 2019

VIDEO: ASHUTUMU UAMUZI WA BUNGE KUTOSHIRIKIANA NA CAG

 

Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe.

KIONGOZI wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, amesema hatua ya bunge ya kutotaka kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, ni kutaka kuwaziba mdomo watu wasitoe maoni yao na kwamba historia italihukumu bunge kwa hatua hiyo.

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai (Chadema) alikuwa  akichangia taarifa ya uamuzi wa bunge uliochukuliwa kufuatia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka iliyotolewa leo bungeni  iliyomhoji  CAG kuhusu kauli yake ya ‘udhaifu wa bunge’ aliyoitoa wakati akihojiwa na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

 

“Historia ambayo mnaiandika leo itawahukumu. Bunge mnajipa utukufu ambao ni wa Mungu pekee, Azimio mnalotaka kulifanya leo dhidi ya CAG mmeshalifanyia kazi?” alihoji Mbowe. na kuongeza kwamba:  “Sisi hapa bungeni tunafanya uamuzi ambao unawaathiri Watanzania, tunataka kupoka haki za msingi za watu kwa sababu sisi tuna mamlaka ya kufanya hivyo.”

 

Ameongeza kwamba katiba inatoa haki na uhuru wa mawazo ambapo kila mtu, akiwamo CAG, ana uhuru wa kutoa maoni na maelezo bila kujali mipaka ya nchi.

 

“Kifungu kilichomtia hatiani (CAG) kinavunja katiba ya nchi. Katika siku za usoni tunapounda kamati za maadili tuangalie kwa makini composition (watu wanaounda kamati hizo),” alisisitiza akisema kwamba kamati iliyopo haiwezi kutoa haki kwa mbunge wa upinzani wala mtu aliye nje ya bunge, watu ambao wanaonekana kuikwaza serikali.

 

Amesema ili maadili ya bunge yasimamiwe sawasawa na kwa haki ni vyema uangaliwe utaratibu wa kufanya uwiano ulio sawa wa wajumbe wa kamati husika.

The post VIDEO: ASHUTUMU UAMUZI WA BUNGE KUTOSHIRIKIANA NA CAG appeared first on Global Publishers.