NEWS

29 Aprili 2019

Watano Wafariki Kimbunga Kenneth, 700,000 Wapoteza Nyumba

SIKU chache baada ya Kimbunga Kenneth kutua nchini Msumbiji, takribani watu 700,000 wanasemekana kuwa wapo  hatarini kupoteza makazi yao katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji, ambapo mvua kubwa imeendelea kunyesha. Watu watano wameripotiwa kufariki kutokana na kimbunga hicho.

 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa hali ya kaskazini mwa Msumbiji ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa, hii ni baada ya siku chache Kimbunga Kenneth kutua nchini humo. Kimbunga hicho kilitua siku ya Alhamisi kwa upepo mkali wenye kasi ya 220km/h (140mph) na kuangamiza vijiji kadhaa.

 

Pemba, mji mkuu wa jimbo la Cabo Delgado ambako kumeshuhudiwa mvua yenye kina cha mita mbili na mafuriko makubwa.

 

Msemaji katika ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinadamu (Ocha), Saviano Abreu, ameeleza kwamba hali ni mbaya katika miji ya Macomia na Quissanga, akiongeza kwamba kuna wasiwasi pia kwa kisiwa kisichoweza kufikiwa cha Ibo. Mawimbi ya hadi mita nne yanatarajiwa, na mashirika ya misaada yanahofia kwamba mvua itazidi kunyesha.

 

“Tuna wasiwasi mkubwa kwa sababu, kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, mvua nzito inatarajiwa kunyesha katika siku nne zijazo,” Deborah Nguyen, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) aliliambia shirika la habari la AFP. na kuongeza:  “Tunatarajia mvua iwe na ukubwa wa mara mbili zaidi ya iliyoshuhudiwa wakati wa kimbunga Idai.”

 

Kimbunga Idai kilisababisha vifo vya watu 900 katika nchi tatu mnamo Machi mwaka huu. Inadhaniwa kwamba watu 400,000 wanaishi Pemba, na mvua kubwa imesababisha watu wengi kuwa katika hatari. Kuna wasiwasi unaotokana na maporomoko ya ardhi katika mtaa wa Mahate mjini humo, na maofisa wa Ocha katika eneo hilo wanasema katika  mtaa wa Natite, nyumba zimeanza kuporomoka.

 

FAO limetakiwa kuanza kutoa misaada kwa watu waliokwama, lakini barabara zilizoharibika zimesababisha shughuli zisitishwe katika maeneo yasiyofikika kirahisi.  Takriban watu watano wamefariki kutokana na kimbunga hicho na takriban nyumba 35,000 zimeharibika vibaya au kubomoka kabisa, maofisa wa kitaifa wanasema.

Maofisa wa uokoaji  kutoka Brazil wamewaokoa watu 350 kutoka sehemu zilizokabiliwa na mafuriko siku ya Jumapili. Hapo jana Jumapili msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameeleza masikitiko yake kutokana na kimbunga hicho.

 

Jimbo la Cabo Delgado halina watu wengi kama eneo lililoathirika na kimbunga Idai na inavyoonekana sehemu kubwa iko katika ardhi ya juu. Tahadhari za mapema kutoka kwa maofisa husika kabla ya kutokea kimbunga hicho huenda ikasaidia kuzuia hasara ikilinganishwa na wakati wa kimbunga Idai.

 

Lakini taarifa zinasema maelfu ya makazi yameharibiwa kutokana na upepo mkali, na eneo hilo linakabiliwa na mashambulio ya wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya Kiislamu katika miezi ya hivi karibuni, jambo ambalo linaonekana huenda likatatiza utoaji wa msaada.

 

LIVE: Rais MAGUFULI Akutana na Prof MWANDOSYA Uso kwa Uso

The post Watano Wafariki Kimbunga Kenneth, 700,000 Wapoteza Nyumba appeared first on Global Publishers.