NEWS

30 Julai 2019

 USIYOYAJUA KUHUSU MATATIZO KATIKA KIZAZI!

K ATIKA matoleo yaliyopita tumeona kwa undani matatizo mbalimbali ya ukeni (Vaginal Diseases) na matatizo katika mlango wa kizazi (Cervical Disorders).  Matatizo ya ukeni husambaa hadi katika mlango wa kizazi kisha huingia ndani katika mfuko wa kizazi na kuleta athari kubwa.

Athari za matatizo ya kizazi

Matatizo ya kizazi yapo mengi kama tutakavyokuja kuona. Athari kubwa za matatizo haya ni maumivu ya kizazi, kutoshika mimba au ugumba na hata kuondolewa kizazi kwa upasuaji ikiwa kama sehemu ya tiba ili kukabiliana na athari za matatizo hayo ya kizazi. Matatizo hutokea zaidi kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa ingawa pia huwapata hata wasichana wadogo na wanawake watu wazima ambao wameshapita umri wa kuzaa.

Matatizo mbalimbali ya kizazi

Kizazi au Uterus imegawanyika katika sehemu kuu tatu kwamba ni sehemu ya chini karibu na mlango wa kizazi (cervical part), sehemu ya kati na pande mbili zinazoungana na mirija.

Kizazi kimeshikiliwa katikati ya nyonga (pelvic) na misuli-mishipa ‘ligaments’ na misuli yenyewe ‘muscles’. Kizazi kina tabaka tatu ambazo ni Endometrium likiwa ni tabaka la ndani kabisa, ‘myometrium’ ambalo ni tabaka la kati na ‘perimetrium’ ambalo ni tabaka la juu au la nje linaloungana na viungo vingine kwa nje kama matumbo, kibofu cha mkojo na mfumo wa haja kubwa.

MATATIZO KATIKA KUTA YA NDANI YA KIZAZI

Hapa mwanamke anaweza kupata maambukizi yanayosababisha tatizo liitwalo kitaalam ‘Endometritis’ au kitalaamu tunasema ‘Inflammation of the endometrium’ ambapo tabaka hilo au kuta hiyo huvimba au kujaa na mwanamke huhisi maumivu ya tumbo chini ya kitovu kwa muda mrefu, kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi au kutoshika ujauzito.

Chanzo cha tatizo hili ni maambukizi yanayojipenyeza ukeni, katika mlango wa kizazi na pia maambukizi huweza kujipenyeza ukiwa katika siku zako au endapo mimba itaharibika au utasafisha kizazi mara kwa mara.

UCHUNGUZI WA TATIZO HILI HUFANYIKA KWA KIPIMO CHA ULTRASOUND.

Tatizo lingine la tabaka hili la ndani ni ‘Endometriosis’ ambapo tabaka hilo hutoka ndani ya kizazi na kukaa au kutokea nje ya kizazi na kukaa au kutokea nje ya kizazi na kusambaa sehemu mbalimbali nje ya kizazi hasa kwenye matumbo hadi kwenye maini.

Tatizo hili humsababishia mwanamke maumivu makali chini ya kitovu ambapo husambaa kiunoni, juu ya tumbo yaani juu ya kitovu na ukiwa kwenye siku zako unapata maumivu makali sana na damu hutoka kidogokidogo. Athari za tatizo hili pamoja na maumivu pia inakuwa vigumu kushika ujauzito.

Saratani ya mfuko wa kizazi

Hii hutokea katika ile tabaka ya ndani ya kizazi au na mara nyingi husababishwa na magonjwa yaitwayo ‘Trophoblastic Diseases’ au ‘molar pregnancy’ ambayo tutakuja kuona kwa undani katika makala zijazo. Magonjwa haya yakiwahi kugundulika hutibika.

Mwanamke mwenye tatizo hili hupatwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu kwa muda mrefu na kizazi huvimba au tumbo kuongezeka ukubwa taratibu, saratani husambaa kwa haraka hadi katika mapafu na kushindwa kupumua vizuri. Tatizo hili huchunguzwa na kutibiwa katika kliniki za magonjwa ya kinamama katika hospitali za mkoa. Athari kubwa ni kupoteza uwezo wa kuzaa na saratani kusambaa haraka mwilini.

The post  USIYOYAJUA KUHUSU MATATIZO KATIKA KIZAZI! appeared first on Global Publishers.