NEWS

1 Agosti 2019

Polisi Yamkana Maalim Seif, Zitto Kabwe Azungumza


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedeyoka amesema jeshi hilo halijavunja kongamano lililoandaliwa na kamati ya maridhiano Zanzibar na kuhudhuriwa na Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT - Wazalendo, Maalim Seif Sharrif Hamadi pamoja na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe.


Sedeyoka amesema kilichotokea ni kwamba askari wa doria walipita eneo hilo na kubaini mkusanyiko wa watu na kutaka warejee kwenye shughuli zao za kila siku inavyokuwa, na kwamba hawakumuondoa Maalim Seif kama ilivyokuwa ikiripotiwa.

Kwa upande wa Zitto Kabwe akizungumza mara baada ya kongamano hilo kuzuiliwa amesema, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Malindi alifika eneo la Kongamano na kutoa amri mbili ikiwemo ya kutaka kumkamata Maalim Seif ama kusimamisha kongamano.

"Hamna mtu ambaye anaweza kuthubutu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumchukua maalim kwa nguvu, tuna wanasheria kuna taratibu za namna za kumhitaji kiongozi mwenye hadhi ya Maalim hawezi tu kuja Mkuu wa Kituo cha Polisi Malindi na kutoa amri. Maalim ni mtu ambaye amekuwa sehemu ya viongozi katika nchi hii, amekuwa Waziri Kiongozi na Makamu wa kwanza wa Rais'', amesema Zitto.

Aidha Zitto amesema kuwa huenda polisi walikuwa na lengo la kuvuruga mkutano na kuzuia Wazanzibar kujadiliana juu ya neema zilizokuwepo wakati wa maridhiano.