NEWS

26 Novemba 2019

Mgombea’ Azikwa, Baba’ke Akataa Ripoti ya Polisi

MAMIA  ya wakazi wa mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang’ mkoani Manyara, wamejitokeza kwa wingi kumzika mkazi wa jijini Arusha, Sirili John Omari,  anayedaiwa kuuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali.



Wakizungumza jana  Jumatatu, Novemba 25 kwenye Kitongoji cha Lamai, Kata ya Katesh, wakazi hao wameiomba serikali kufanya uchunguzi juu ya kifo hicho wakisema kifo hicho ni cha kikatili na huenda kinahusisha mambo ya kisiasa.



Baba mzazi wa marehemu, Mzee John Omari, amesema hana imani na taarifa iliyotolewa na polisi juu ya mazingira ya kifo cha mtoto wake akisema polisi wanadai kuwa kuna uwezekano Sirili alijiua mwenyewe wakati mazingira ya tukio hilo yanaonyesha kuwa aliuawa.



Diwani wa Katesh, Peter Lowri ambaye msiba ulikuwa kwenye kitongoji cha eneo lake la Lamai amesema Sirili ameuawa kikatili.

“Nilikagua mwili wake na kukuta ameuawa kikatili, nadhani alipigwa na shoka kwenye mabega yote mawili na kifuani, ni kifo cha kikatili kwelikweli,” amesema Lowry.




Katekista wa Kanisa Katoliki Katesh aliyeendesha ibada hiyo, Victoria Charles, amewaasa waumini walioshiriki ibada hiyo ya mazishi kutowazia kulipa kisasi kwa jambo lolote lile maishani.



Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amesema polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho.

“Hao wanaohusisha hicho kifo na masuala ya kisiasa wana lao jambo; tumefuatilia Kata ya Unga Ltd na marehemu Sirili hakuwahi kuchukua fomu ya kugombea lolote kupitia chama chochote,” amesema Kamanda Shana.



Marehemu Sirili ambaye alizaliwa Desemba 10, 1998 kwenye Kata ya Katesh na kufariki jijini Arusha, Novemba 21, hajaacha mke wala mtoto.