Faru Fausta, ambaye anaaminika kuwa ndiye faru mzee zaidi duniani amefariki akiwa na miaka 57 hapa nchini.
Fausta ameishi maisha yake yote katika Hifadhi ya Ngorongoro mpaka umauti ulipomkuta jana Ijumaa, Disemba 27.
Fausta ameishi maisha yake yote katika Hifadhi ya Ngorongoro mpaka umauti ulipomkuta jana Ijumaa, Disemba 27.
Mhifadhi mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) Dkt Freddy Manongi asema Fausta ndiye alikuwa faru mzee zaidi duniani, hiyo ni historia kwa Tanzania.
"Tunahisi kifo chake ni cha kawaida kutokana na umri wake mkubwa. Madaktari wapo njiani watatueleza hasa sababu ya kifo chake baada ya kufanya vipimo," ameeleza Manongi.
Faru huyo jike alikuwa chini ya uangalizi maalumu kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita baada ya afya yake kudhoofu na kuanza kushambuliwa na wanyama wakali mwituni.
"Wanyama wakali hususani fisi walianza kumshambulia na akapata vidonda vikubwa sana. Ilipofika mwaka 2016 ilibidi tumtoe porini na kumuweka kwenye uangalizi maalumu. Vidonda vyake vilipona lakini afya yake bado ilikuwa dhoofu hatukuweza kumrejesha porini." alisema.
Faru Fausta licha ya umri wake mkubwa hakuwahi kuzaa na hiyo inaelezwa kuwa huenda ikawa ni moja ya sababu ya kuishi kwake kwa muda mrefu.
Faru wanakadiriwa kuweza kufikisha umri wa miaka 37 mpaka 43 wakiwa porini na huweza kufikisha mpaka miaka 50 wakifugwa katika maeneo maalumu.