NEWS

28 Desemba 2019

Urusi yazindua Mfumo Mpya wa Kombora Lenye kasi zaidi ya Sauti la 'Avangard Hypersonic'



Shirika la Habari la Itar-Tass la Russia limeripoti kwamba jana Ijumaa Sergey Shoygu, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo alizindua mfumo wa kwanza wa makombora ulio na kasi kubwa kuliko sauti.

Kwa mujibu wa shirika hilo la habari shughuli ya uzinduzi wa mfumo huo, ilifanyika majira ya saa 10 asubuhi kwa majira ya Moscow, mji mkuu wa nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo Jumamosi iliyopita pia Rais Vladmir Putin wa Russia na katika kikao kilichohudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo akiwemo Sergey Shoygu, Waziri wa Ulinzi, alisema kuwa kinyume na huko nyuma katika harakati za ushindani na Marekani, kwa mara ya kwanza katika historia yake, Russia imefikia kiwango cha juu katika uundaji wa zana mpya za kivita.

Akibainisha suala hilo Putin alisema: "Tumefikia kiwango cha uwezo wa kijeshi cha zama hizi, na hivi sasa ni Marekani inayopigania kuweza kutufikia. Hakuka nchini yenye silaha za Hypersonic, achilia mbali silaha za Hypersonic za kuvuka mabara."

Akizungumzia makombora ya Avangard hypersonic alisema kuwa, makombora hayo ya kuvuka mabara yanaweza kwenda umbali wa anga ya dunia kwa kasi ya mara 20 zaidi ya sauti sambamba na kuvuka aina yoyote ya ngao ya kiulinzi iliyopo duniani.

Akizungumzia suala la kuongeza askari kunakofanywa na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO katika mipaka ya magharibi mwa Russia na kitendo cha Marekani cha kujiondoa kwenye mapatano ya makombora ya masafa ya wastani yaliyotiwa saini mwaka 1987, Rais Putin alisema kuwa ni lazima Russia imiliki silaha za kisasa duniani.