NEWS

30 Aprili 2020

Taifa Tutenge Wiki Moja, Tupige ‘Nyungu’ Kwelikweli



SERIKALI imewataka wananchi wasisite kutumia njia mbadala ambazo zitaweza kuwasaidia katika janga hili la corona, ikiwemo kujifukiza, kwani utaratibu huo wa nyungu upo katika makabila mbalimbali nchini na umekuwa ukitumika tangu enzi za mababu.

Jafo amesema hayo jana wakati akizungumza na wanahabari kuhusu mpango wa taifa wa kufundisha wanafunzi kwa njia za kieletroniki katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona yaliyosababisha shule na vyo vyote nchini kufungwa.

“Niwaombe Watanzania kama kuna watu wanatutangazia kuwa kuna mbinu inaweza kutusaidia katika janga la corona na ni mbinu sahihi, nimeona watu wakisisitiza kuhusu kujifukiza sisi kule kwetu tunasema mtu unamuweka ‘Nyungu’ watu wasione aibu piga nyungu kweli kweli.

“Huu utaratibu upo hata kwenye makabila yetu, weka chungu chako vizuri, weka moto wako, weka majani ya mti wako unaoujua yachemke kweli kweli jifunike na shuka hata blanketi jikoleze utoke jasho kweli kweli tumia mbinu zote.


“Tusione aibu tukasema hili suala ni la waganga wa kienyeji, hakuna! tumieni vyakula vinavyotakiwa bila kuona aibu, jifukishe nyungu na hata ikiwezekana tukiamua kama Taifa tungetenga wiki moja ya nyungu nchi nzima.


“Tungetenga wiki moja ya nyungu, mgonjwa, mzima wiki nzima, asubuhi nyungu, mchana nyungu na jioni nyungu na kula vyakula vya kurutubisha mwili wiki nzima zoezi maalumu, inawezekana ingekuwa mkakati mkubwa wa nchi yetu kwa ajili ya kuliokoa taifa letu.

“Hili jambo lingefanyika Marekani au Ulaya, Mataifa yote ya Afrika yangeiga na yangetangaza wiki ya nyungu lakini hawaja tangaza watu weupe, hivi sisi tunashida gani? yani jambo likitoka kwetu sisi sio jambo.


“Naomba niwaambie jambo inawezekana watu wengine tungewaokoa kwa namna hiyo, ingekuwa haijalishi mtu anaumwa haumwi ni wiki ya nyungu tena mimi ningefurahi kina baba ndo wangekuwa wa kwanza kupika hizo nyungu vizuri,” amesema Jafo.