NEWS

14 Septemba 2020

Baada ya Wasafi FM kufungiwa Daimond aishukuru TCRA



Nyota wa muziki nchini, msanii Diamond Platnumz ambaye pia ni Mkurugenzi wa Wasafi Media ameishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuwapa nafasi ya kujifunza zaidi.
Kauli ya Diamond inakuja baada ya TCRA kusitisha utoaji huduma za utangazaji kwa Wasafi FM kwa muda wa siku saba kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 18 mwaka huu.

Akizungumza hilo kupitia Big Sunday Live ya Wasafi TV, Diamond amesema adhabu hiyo ni kuwapa nafasi ya kujifunza kama kituo cha habari kinachotazamwa zaidi kwa sasa nchini.

Aidha, ameeleza kipindi adhabu hiyo itakapomalizika watarejea kwa uweledi zaidi na kuisadia serikali kuelimisha jamii kwa lengo la kuandaa kizazi bora cha hapo baadaye chenye maadili.

Uamuzi wa kufungiwa Wasafi FM ulitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba jijini Dar es Salaam ambapo alisema hatua hiyo ni kutokana na kituo hicho kukiuka kanuni namba 11 ya Kanuni za Mawasiliano ya kielektroniki na Posta ya mwaka 2018. Mhandisi Kilaba alisema kuwa ukiukwaji huo wa kanuni ulifanyika katika vipindi vya "The Switch" na "Mashamsham".