NEWS

30 Septemba 2020

Marekani Yampa Shavu Mondi



HUJATAJWAhata na mkuu wa mkoa, msanii unavimba kichwa! Sikia hii: “Serikali ya Marekani yampa shavu msanii Diamond au muite Nasibu Abdul a.k.a Mondi.


Kapu la stori za sanaa mwishoni mwa wiki iliyopita, lilijaa ishu kubwa ambayo Risasi liliinyaka kwamba, baada ya Diamond kufanya kolabo ya heshima na msanii wa Marekani, Alicia Augello Cook ‘Alicia Keys’, ubalozi wa nchi hiyo Bongo, umetoa shavu kwa Mondi kwa kuandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Great to see American artist @aliciakeyscollaborate w/Tanzanian artist @DiamondPlatnumz.”



 

Ambapo kwa Kiswahili ubalozi huo uliandika: “Inafurahisha kuona msanii @aliciakeys akimshirikisha msanii wa Kitanzania, @diamondplatnumz.”


Jicho la mwandishi limebaini kuwa ‘Twiti’ hiyo ya ubalozi wa Marekani nchini, unaoongozwa na balozi Donald Wright, ni ya kipekee kwa Mondi na kwamba inawasha taa ya kijani kwa msanii huyo kutamba kimataifa.


CHANZO CHA PONGEZI NI HIKI


Chanzo cha pongezi za Marekani kwa Mondi, ni baada ya msanii huyo wa Bongo kushirikishwa na staa huyo wa muziki wa Marekani katika wimbo wake wa Wasted Energy, ambao unapatikana katika Albam mpya ya Alicia Keys iitwayo Alicia, ambayo aliifyatua Ijumaa, Septemba 18, mwaka huu.


Katika wimbo huo wa Wasted Energy, mtoto wa Tandale alitupia mashairi yake kwa Lugha ya Kiswahili, jambo ambalo wengi wamempongeza kwa kusema ameijenga heshima ya Tanzania kimataifa.


Kionjo cha mistari ambayo Mondi alimuonjesha msanii huyo wa kike mwenye mvuto wa Marekani, ni:“Kwa nini penzi umelikata miguu,Unalibidua mara chini mara juu?Why? (Kwa nini?)Why? (Kwa nini?)Moyo unaumia, Moyo unaumia Moyo unaumia kwa nini unaugeuza nguo karaha?


Eti karaha, oh-oh,” yaani kama hivyo tu mzee baba; huku Alicia Keys yeye akitiririka sehemu ya mashairi yake kama ifuatavyo:


“Too many times, you turned a blind eye to the way I feel Oh, you’re the reason why I’m numb And when I try to give you my time, it’s never, ever ideal Had to learn it the hard way, oh yeah,” akimaanisha hivi kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili:


“Mara nyingi sana, ulifumbia macho jinsi ninavyohisi Ah, wewe ndio sababu nimeshikwa na ganzi,Na ninapojaribu kukupa wakati wangu, sio bora kabisa, Ilibidi nijifunze kwa njia ngumu, oh ndio.”


FAIDA KWA MONDI KWA KUTAJWA NA MAREKANI


Macho ya watazama mambo ya muziki kwa kina, yanaona kwamba kitendo cha Mondi kushirikishwa na Alicia Keys na kupewa heshima na ubalozi wa Marekani, kitamfanya msanii huyo kujulikana zaidi kimataifa, jambo ambalo lina faida kubwa kwake.


“Naona muziki wetu unakua sasa, kama wasanii wa Marekani wanaomba kolabo na sisi, hii ni hatua kubwa, hongera Diamond.”


“Mzee jiandae kwa shoo za kufa mtu baada ya Corona kuisha.”“Hii ni level nyingine kabisa ya Diamond, ila kuna wengine bado wanamchukulia poa, wakati dogo (Mondi) kapasua anga za Trump (Donald, rais wa Marekani).Hizo ni baadhi ya komenti ambazo zilitupia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kusherehesha kile alichoki-skoo kibabe mtoto wa Tandale.


REKODI TATU ZA KIPEKEE


Uchunguzi unaonesha kuwa, tukio la Mondi kushirikishwa na staa huyo wa Marekani, kumemfanya msanii huyo kuweka rekodi tatu kibabe.


Rekodi ya kwanza aliyoweka Mondi ni kwamba, anakuwa msanii wa kwanza Bongo kuombwa, rudia tena “kuombwa”, siyo kuomba kolabo kwa msanii huyo mkubwa; kama ambavyo wasanii wengine huwa wanafanya; usichanganye madawa.


Nyingine ya ajabu ambayo ameiweka Mondi ni ile ya msanii kutoka Bongo kufanya kolabo hiyo na msanii nyota wa Marekani na wimbo wake kuingizwa kwenye nyimbo zinazokamilisha Albam kwa Bongo haijapata kutokea.Rekodi ya tatu ni kitendo cha ubalozi wa nchi kubwa kama Marekani kupongeza ushirikiano wa msanii wa nchi yake kufanya kolabo na msanii wa Bongo.


ALICIA KEYS ALIVYOANZA KUMZIMIA MONDI


Mapema wiki hii, Keys alitupia orodha ya nyimbo anazopenda kuzisikiliza ukiwemoNana ambao Mondi amemshirikisha staa wa Nigeria, Mr Flavour.


Kama hiyo haitoshi, alisikiliza pia Wimbo wa African Beauty ambao Mondi amemshirikisha staa wa Marekani, Omarion, hiyo ni kuonesha kuwa msanii huyo wa Marekani alianza kumkubali Mondi kitambo.


Kama hilo alitoshi mapema mwaka huu, mume wa Alicia Keys, Beatz naye aliposti wimbo wa Gere wa Mondi alioshirikishwa na aliyekuwa mwandani wake, Tanasha Donna ambapo alisema anatamani kuufanyia remix wimbo huo.


ALICIA KEYS NI NANI?


Alicia Keys ni mrembo, staa wa muziki wa R&B kutoka pande za Marekani, ambaye ana umri wa miaka 39. Amesumbua na ngoma zake kali ikiwemo No One ambayo ilikamata namba moja katika chati za Hot 100.


Wimbo huo ulikuwa kwenye Albam yake iliyofahamika kwa jina la As I Am, ambayo iliitoa mwaka 2007 na kusimama namba moja kwenye Billboard 200 nchini humo na kuuza kopi 742,000 kwa wiki ya kwanza.Hii ina maana kwamba, Alicia Keys siyo msanii wa kispotispoti ukilinganisha na wasanii wa Bongo.


NI SOMO KWA HARMO, KIBA NA ZUCHU


Katika kitu ambacho kinaonesha kuwa Wabongo wamekuwa na kiu ya kuona vitu vyao vinapenya kimataifa, waliwatolea mwito wasanii wengine kama Ali Kiba, Zuhura Othman ‘Zuchu’ na Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ nao kuzidi kukaza buti, ili nao wapenye zaidi kimataifa.


“Umefika muda wa kuelewana, Wabongo tuzidi kuongeza sauti kwenye vitu vyetu, iwe michezo, sanaa na mambo mengine, ili tutoke kimataifa.”


“Kazi kwenu wasanii wengine Bongo, mkichukulia ishu ya Mondi kichawi mtaishia kununa, lakini mkiichukulia positive, mtakaza buti ili nanyi mpite njia anayotoboa Diamond.”


Baadhi ya komenti zilizotupiwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu ishu ya Mondi na pongezi za ubalozi wa Marekani.