NEWS

30 Septemba 2020

Mfanyakazi Tanesco Adaiwa Kumkata Kiganja Mkewe



MFANYAKAZI wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) jijini Dar es Salaam, Ombeni Alfayo anadaiwa kumkata mkewe, Veronica Kidemi (30), kiganja cha mkono wa kulia kwa madai ya wivu wa mapenzi. Veronica ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kiranyi na mkazi wa Kijiji cha Siwandet.


Kwa sasaVeronica amelazwa Hospitali ya Selian wilayani Arumeru mkoani hapa na anadai amepigwa na mumewe kutokana na wivu wa mapenzi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo saa 11:45 jioni juzi Siwandeti Kata ya Kimyaki Tarafa ya Enabosihu wilayani Arumeru.



 

Kamanda Hamduni alisema Veronica alijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali mikono yake miwili na mumewe, Alfayo ambaye ni mfanyakazi wa Tanesco, na kusababisha kiganja cha mkono wa kulia kutengana na sehemu nyingine ya mkono.


Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo, ingawa taarifa za awali zinadai ni wivu wa mapenzi.


Alisema mtuhumiwa alitoroka baada ya kufanya tukio, lakini amekamatwa jijini Dar es Salaam. Veronica alidai mumewe amekuwa na tabia ya kumtukana na kumpiga kwa vitu vyenye ncha kali na wakati mwingine alimnyang’anya watoto wao wawili.


Alidai Septemba 26, mwaka huu alitoka kazini saa 11:00 jioni na kwenda Mianzini kutoa fedha na kununua mahitaji ya kifamilia na baada ya hapo aliwenda nyumbani kupika.


Alidai baada ya kufika nyumbani, mumewe alikuwa yupo ndani, alianza kumtusi huku akimkata kwa panga na katika kumkwepa aligundua kiganja cha mkono wake wa kulia kimekatwa.


Veronica alidai vikao vya kifamilia vimekuwa vikifanyika na hata kwa viongozi wa dini wamesuluhisha. Lakini, mara kwamara amekuwa akipigwa na baada ya kipigo ananyang’anywa watoto.


“Mume wangu amekuwa na wivu sana na nimepata vipigo mara kwa mara; na pia nimekuwa nikinyang’anywa watoto wangu.


Ninachoomba serikali inisaidie nipate watoto wangu, amekuwa akinidhalilisha sana, huyu mume ananinyima hata kuongea na ndugu zangu,” alidai mwalimu huyo.