NEWS

12 Novemba 2020

Alichokisema Majaliwa Baada ya Kuidhinishwa na Bunge

 


By Peter Elias, Mwananchi pelias@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atafanya kazi na wabunge wote bila kujali itikadi za vyama na kusisitiza kuwa hata mawaziri na naibu mawaziri watakaoteuliwa nao watafanya kazi na wabunge wote.


Majaliwa amesema hayo leo Alhamisi Novemba 12, 2020 punde baada ya kuidhinishwa na Bunge kwa kupigiwa kura 350 za ndio sawa na asilimia 100.


Majaliwa amesema atafanya kazi kwa moyo na pia amemuhakikishia Rais John Magufuli kwamba atakidhi matamanio yake huku akimshukuru kwa kumteua akiahidi kufanya kazi zaidi ya kuwaletea maendeleo Watanzania.


Amemshukuru Rais Magufuli kwa imani kubwa aliyonayo kwake kwa kuendelea kumwamini,  kwamba anaweza kuendelea kufanya yale aliyoyafanya miaka mitano iliyopita au zaidi katika kipindi kingine.


“Niendelee kumhakikishia kwamba matamanio yake ya kuamua kulitoa jina hili mbele ya Bunge tukufu…, hiyo ni imani kwamba nitafanya kazi kwa ufanisi zaidi,” amesema Majaliwa huku akishangiliwa na wabunge.


Amewashukuru pia wabunge akisema wamemfanyia jambo kubwa yeye na familia yake na kwamba idadi ya kura zao imemfariji.


 

“Tuna wabunge pia kutoka vyama rafiki, vyama vya upinzani. Kura asilimia mia moja maana yake nao wamepiga kura ya ndiyo. Ninawashukuru sana.”


“Nitapita tena kwenye maeneo yenu yote kupata fursa kuona shughuli za maendeleo ambazo wenzangu mnazisimamia, tutapita kwenye majimbo yenu kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua. Niwahakikishie kuwapa ushirikiano hapa bungeni,” amesema Majaliwa.


Amesema ataendelea kupokea ushauri wao pamoja na changamoto zao na kuziwekea mkakati wa namna ya kuzitatua.


Waziri Mkuu ametoa shukrani kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia uteuzi wake ili aendelee kufanya kazi ya kuliletea maendeleo Taifa.


Amempongeza pia Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa ushindi alioupata katika jimbo lake la Kongwa na kuchaguliwa tena kuwa Spika wa Bunge la Tanzania.


“Hakuna siri kwamba umefanya kazi nzuri sana kama Spika wa Bunge hili katika kipindi cha miaka mitano hongera sana mheshimiwa Spika.”


“Tuna imani kwamba kazi uliyoifanya katika kipindi kilichopita, utaendelea kuifanya katika kipindi kingine Serikali tutaendelea kukupa ushirikiano,” amesema Majaliwa.