NEWS

21 Januari 2021

China yamuwekea vikwazo Pompeo na maafisa wenzake 27 wa Marekani


China imewawekea vikwazo Maafisa 28 waliokuwa kwenye utawala wa Rais Trump akiwemo Waziri wa Mambo ya nje aliemaliza muda wake, Mike Pompeo, taarifa toka Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema maafisa hao walikiuka haki ya China kama taifa huru.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya China kuhusiana na uamuzi huo imetolewa huku Joe Biden akiapishwa hapo jana kuwa rais mpya wa Marekani na kuhitimisha enzi za utawala wa Trump 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mbali na Mike Pompeo, maafisa wengine waandamizi wa serikali ya Trump waliomo kwenye orodha hiyo ya vikwazo ni pamoja na mshauri wa masuala ya biashara Peter Navarro, mshauri wa usalama wa taifa Robert O'Brien, naibu waziri wa mambo ya nje wa masuala ya Asia Mashariki na Pasifiki David Stilwell, waziri wa afya Alex Azar na balozi wa Marekani Umoja wa Mataifa Kelly Craft.

Beijing imemwekea vikwazo pia mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa serikali ya Trump John Bolton na Stephen Bannon aliyewahi kuwa mshauri wa rais huyo wa Marekani aliyemaliza muda wake.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeeleza katika taarifa yake hiyo kwamba, kwa sababu ya maslahi binafsi ya kisiasa, chuki na mtazamo mbaya dhidi ya China, maafisa hao 28 wa serikali ya zamani ya Marekani hawakuonyesha kujali maslahi ya watu wa mataifa ya China na Marekani.

"Watu hawa na jamaa wa karibu wa familia zao wanapigwa marufuku kuingia ardhi kuu ya China, Hong Kong na Macao", imesisitiza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu hao, makampuni na taasisi zenye mfungamano nao haziruhusiwi pia kufanya biashara na China..