NEWS

21 Januari 2021

Rais Magufuli atunukiwa Tuzo kwa kuendeleza Kiswahili


Rais Dkt John Magufuli ametunukiwa tuzo ya Juu ya Shaaban Robert kutokana na mchango wake katika kukuza na kuendelea lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.

Dkt Magufuli ametunukiwa tuzo hiyo jana  jijini Dodoma baada ya kupendekezwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Baraza la Kiswahili la Zanzibar(BAKIZA), taasisi, idara na vyama mbalimbali vya Kishwahili nchini.

Tuzo hiyo hutolewa kwa mtu aliyendika kitabu/vitabu vya kishwahili, kwa kuangalia mchango wa mhusika katika kuendeleza lugha hiyo Kitaifa na Kimataifa.

Pia huangaliwa mchango wake katika uchapishaji wa vitabu vingi vya lugha ya Kiswahili, mchango wake katika mabadiliko chanya katika maendeleo ya lugha hiyo, lakini vile vile huangaliwa mchango wake katika uongozi wa masuala mbalimbali yahusuyo Kiswahili.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli amechukua hatua mbalimbali zilizowezesha kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili na hivyo kuchangia kutunukiwa tuzo hiyo.

Kwanza ni marekebisho ya Sheria ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ya mwaka 1967 ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa kupitwa na wakati, marekebisho yaliyoiwezesha BAKITA kufanya kazi kwa urahisi na ufanisi zaidi.

Sifa nyingine iliyochangia ni mchango wake kukuza Kiswahili Kusini mwa Afrika ambapo mwaka 2019 alipofanya ziara nchini Zimbabwe na Namibia alisisitiza matumizi ya lugha hiyo na kuahidi kuwa Tanzania itatoa Walimu kufundisha Kiswahili katika nchi hizo.