WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wote wa Sekta za umma na binafsi wanatakiwa waendelezwe kitaaluma kwa ajili ya kukuza weledi, ubunifu na maadili ili waweze kusimamia ipasavyo maendeleo na kuongeza tija na mapato ya Taifa.
Amesema katika kipindi hiki ambacho nchi imeingia katika uchumi wa kati, Serikali ingependa kuona nguvukazi katika ngazi mbalimbali inaimarishwa na kuhakikisha viongozi wanatumia ujuzi na weledi katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu, rasilimali fedha na miradi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 29, 2021) katika Mahafali ya Wahitimu wa Programu ya Uanagenzi kwa Maafisa Watendaji Wakuu (Ceo Apprenticeship Program) yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro, Dar-Es-Salaam.
“Dhana ya uanagenzi ni suluhisho la kuhakikisha wataalamu wetu wanajengewa ujuzi unaohitajika mara kwa mara ili kuwaongezea umahiri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Nchi inahitaji viongozi wanaoongoza kwa vitendo na kuwa mfano bora kwa Taifa.”
Waziri Mkuu amesema pamoja na mambo mengine, dhana ya uanagenzi inalenga kukuza mtandao wa viongozi kupitia mafunzo kwa vitendo na ushauri ili kuwawezesha viongozi au maafisa watendaji wakuu kufanya maamuzi yenye maslahi mapana kwa Taifa.
Amesema ana imani kwamba wahitimu hao watakuwa watendaji wenye uwezo wa kusimamia mabadiliko, wasikivu, waadilifu na wenye mori ya kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali wanazozifanyia kazi.
Waziri Mkuu amesema manufaa na faida za ujenzi wa uwezo wa wataalam wa ndani hususan viongozi na maafisa watendaji wakuu ni pamoja uwepo wa rasilimali na nguvu kazi ya Taifa yenye ubora wa ujuzi, weledi na umahiri wa hali ya juu unaowawezesha kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
Amesema manufaa mengine ni nchi kuwa na viongozi na watendaji wakuu wabunifu, wenye maadili na uzalendo ambao wapo tayari kujenga uchumi imara, endelevu na unaokua pamoja na kukuza uwezo wa kitaalam na ujuzi wa matumizi ya teknolojia mpya ya kidijitali.
Akizungumzia kuhusu sekta binafsi, Waziri Mkuu amesema Serikali inathamini sekta binafsi kwa kuwa ina nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi. “Hivyo kwa viongozi hawa kupata mafunzo haya itasaidia kusimamia nguvukazi yenye ujuzi na maarifa itakayozidi kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.”
“Ni ukweli usiopingika kuwa, sekta binafsi na asasi za kiraia zikiwemo taasisi za dini zimekuwa zikitoa mchango muhimu katika kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu, maarifa na ujuzi nchini. Hivyo, napenda kutambua na kupongeza mchango wa sekta binafsi katika kuwajengea uwezo Watanzania kielimu, maarifa na uwezo wa kuongoza katika nafasi za juu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Bodi ya Wakurugenzi wa CEO Roundtable of Tanzania na Taasisi ya Uongozi washirikiane ili kubaini maeneo yenye uhitaji na kutoa mafunzo yenye tija. Amesema anatambua Taasisi ya Uongozi inaendesha programu za mafunzo ya uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Alto cha Nchini Finland.
Waziri Mkuu amesema ushirikiano huo utaleta tija na utaondoa marudio na kuimarisha ubunifu katika kutoa mafunzo na kuleta manufaa kwa washiriki wa mafunzo hayo. Pia amewataka waandae mipango ya mafunzo yenye lengo la kutambua na kujenga uwezo wa Watanzania katika sekta za kipaumbele, hususan sekta ya madini, mafuta na gesi, ujenzi na TEHAMA.
Pia, Waziri Mkuu amewataka washirikiane katika kuwajengea uwezo wa wataalam wabobezi katika masuala ya uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere na mradi wa reli ya kisasa (SGR) na usimamizi na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki litakaloanzia Hoima, nchini Uganda hadi Chongoleani, Mkoani Tanga.
Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Maafisa Watendaji; Wakuu Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania – CEOrt); Sanjay Rughani alisema mafunzo hayo ya Uanagenzi kwa Maafisa Watendaji Wakuu yanalenga kuwaandaa Watanzania kushika nafasi za juu za kiuongozi na kiutendaji katika taasisi mbalimbali.
Mkurugenzi huyo alisema mpango huo wa mafunzo kwa Maafisa Watendaji Wakuu umedhamiria kuwajengea Wataalam wa Kitanzania uwezo mkubwa ili waweze kushindana katika kuhudumu kwenye nafasi za Utendaji Mkuu katika Taasisi, Programu na miradi mikubwa ya Kitaifa na kimataifa.