Rais Magifuli pia ametaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutokubali kila chanjo inayoletwa hapa nchini bila kuwa na uhakika nayo.
Akihutubia wananchi katika kijiji cha Butengo wilayani Chato katika hafla ya uzinduzi wa shamba la miti Silayo, Rais Magufuli amesema, hana mpango wa kutangaza kufungia watu ndani kutokana na tishio la maambukizi ya ugonjwa wa corona na kuwataka Watanzania kuchapa kazi.
Aidha amewataka wananchi wasitishike na maneno kuwa corona itarejea tena kwani tayari Mungu yupo pamoja na watanzania.
“Mtatishwa sana ndugu zangu Watanzania lakini simameni imara, najua wapo baadhi ya watanzania hata wameondoka ndani ya nchi na kukimbilia maeneo mengine na kwenda kuchanjwa na walikochanjwa huko wamekuja huku wametuletea corona ambayo ni ya ajabu ajabu simameni imara.
“Chanjo hazifai kama Wazungu wangekuwa na uwezo wa kuleta chanjo, hata chanjo ya Ukimwi ingekuwa imeshaletwa, chanjo ya kifua kikuu ingekuwa kifua ingeshaondoka, hata chanjo ya malaria ingekuwa ishapatikana hata chanjo ya kansa ingekuwa imeshapatikana, lazima watanzania tuwe waangalifu kwa mambo ya kuletewa letewa,” amesema Rais Magufuli.
“Sisi Watanzania hatujajifungia ndani na hatutegemei kujifungia ndani, na wala sitegemei kutangaza hata siku moja kwamba tunajifungia ndani kwa sababu Mungu wetu yupo hai na ataendelea kutulinda Watanzania.
“Tutaendelea kuchukua tahadhali nyingine za kiafya ikiwa pamoja na kujifukizia, unajifukizia huku unamuomba Mungu unasali…, sali huku unapiga zoezi la kulima mahindi, viazi ili ule vizuri ushibe. Corona ashindwe kuingia katika mwili wako,” ameongeza Rais Magufuli.