Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema alimuamini zaidi rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli na ndio maana alimteua kuwa waziri katika wizara tatu tofauti katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake akisema, “alikuwa jembe langu.”
Kikwete aliyekuwa rais mwaka 2005 hadi 2015 ameeleza hayo leo Ijumaa Machi 26, 2021 katika ibada ya mazishi ya kiongozi huyo inayofanyika wilayani Chato Mkoa wa Geita nchini Tanzania.
Kikwete ambaye kwa nyakati tofauti alimteua Magufuli kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ujenzi amesema kiongozi huyo alikuwa jembe lake alilolitegemea ndiyo maana alimuweka kwenye wizara tatu ngumu.
“Nilianza na wizara ya ardhi nilimwambia kule kuna wala rushwa, wanagawa viwanja mara nne nne, wale ni watu wagumu mno nikamwambia akawanyooshe.”
“Akaenda kufanya kazi kubwa akawanyoosha, akajitahidi lakini wale watu ni wagumu mno, Rais ukifanikiwa kuibadilisha wizara ya ardhi watu watashukuru,” amesema.
Amesema baada ya kufanya kazi hiyo vizuri alimuhamishia wizara ya mifugo ambako nako aliiendesha vyema wizara hiyo.
Kikwete alieleza kuwa katika miaka mitano ya mwisho ya uongozi wake alimuhamishia Magufuli wizara ya ujenzi ili aweze kuiunganisha mikoa yote kwa barabara za lami.
“Miaka mitano ya mwisho nilitaka kufanya kitu ambacho kitaacha alama na niliona kuunganisha mikoa ndiyo kitu muhimu nikamkabidhi kazi hiyo Magufuli.”
“Tumeona sasa hivi mikoa karibu yote imeunganishwa kwa barabara kama imebaki ni michache, alifanya kazi hiyo kwa ufanisi,” amesema Kikwete.
Aidha Mhe.Dkt.Kikwete amesema katika mchakato wa kupitisha majina ya wagombea Urais 2015 hakuweza kusita kulichagua jina la Magufuli kwani alifahamu fika utendaji kazi.