Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa, kwa sasa kimbunga hafifu Jobo hakipo nchini Tanzania.
Taarifa ya TMA iliyotolewa saa chache zilizopita imeeleza kuwa, hakuna madhara ya moja kwa moja yanayotarajiwa kutokana na kimbunga hicho hafifu.
Hata hivyo imesema kuwa, masalia ya mawingu yanayoambatana na kilichokuwa kimbunga Jobo yanaweza kusababisha mvua katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Haki ya Hewa Tanzania, mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yamesambaa baharini karibu na maeneo ya kusini mwa pwani ya Tanzania na Msumbiji.
TMA imewashauri Wananchi wote kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka mamlaka hiyo, pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika.